Viongozi wa kundi la BRICS watia saini tamko la pamoja
26 Julai 2018China, Urusi, Brazil, India na Afrika Kusini zimeapa kupambana na sera ya kulinda biashara wakati ambapo vitisho vya ushuru kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump vinaongezeka.
Katika tamko lao la pamoja viongozi hao wamesema wanatambua kwamba mfumo wa kibiashara wa kimataifa unakabiliwa na changamoto zisizokuwa za kawaida na wamesisitiza juu ya umuhimu wa uchumi wa dunia ulio wazi.
Rais wa China Xi Jinping amewataka viongozi wenzake wa nchi zinazoinukia kiuchumi kuikataa kabisa sera ya kuweka vizingiti kwa lengo la nchi kuzuia ushindani katika biashara kwenye mkutano huo wa mwaka wa viongozi wa nchi hizo maarufu kama Brics unaofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Marekani imelaumiwa kwenye mkutano huo kwa sera yake ya kuzitoza ushuru mkubwa bidhaa kutoka nje.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Geng Shuang amesema wito wa nchi zinazoendelea ni wa kutaka ziwe sehemu ya jitihada za jumuiya ya kimataifa za kudumisha utawala wa kimataifa na kuchangia jukumu la kuimarisha ukuaji wa uchumi duniani.
Vita vya kibiashara vinavyoendeshwa na Marekani dhidi ya China, taifa la pili kwa nguvu za kiuchumi duniani, na pia dhidi ya washirika wake wakubwa muhimu, ni suala linalozingatiwa kwa makini kwenye mkutano huo kwa lengo la kujenga mshikamano ili kuunga mkono kile ambacho rais wa China anakiita neema ya pamoja.
Viongozi hao wa Brics, rais wa China Xi Jinping, rais wa Urusi Vladimir Putin, rais wa Brazil Michel Temer, waziri mkuu wa India Narendra Modi na mwenyeji wao rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa katika siku ya pili ya mkutano huo walisimama pamoja kwa ajili ya kupiga picha huku wakiwa wameshikana mikono. Rais wa Uturuki Recep tayyip Erdogan pia amealikwa kwenye mkutano huo.
Siku moja kabla ya mkutano huo, rais wa China alisema dunia inakabiliwa na changamoto ya kuchagua kati ya ushirikiano na mapambano wakati ambapo mgogoro wa biashara na Marekani umepamba moto huku akionya kuwa hakutakuwa na mshindi.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwa upande wake, ameunga mkono wazo la kufungua matawi ya kikanda ya Benki ya Maendeleo Mpya kwa wanachama wa BRICS. Putin amesema wanajadiliana na Brazil juu ya suala hili na kwamba baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo juu ya suala hili, ufunguzi wa ofisi za benki hiyo utaanzia nchini Urusi.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu