1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya Rais Nkurunziza haijulikani baada ya mapinduzi

14 Mei 2015

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo kuijadili Burundi baada ya jenerali mwandamizi wa jeshi nchini humo kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunzinza kutoka madarakani.

https://p.dw.com/p/1FPYJ
Picha: B. Smialowski/AFP/GettyImages

Ufaransa ndiyo imeitisha kikao hicho cha dharura ambacho kitafanyika hii leo punde tu baada ya wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Iraq.

Hapo jana Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye alikuwa mkuu wa shirika la ujasusi nchini Burundi, alitangaza kuwa utawala wa Rais Pierre Nkurunzinza umepinduliwa na jeshi kutoka madarakani kwa kukiuka matakwa ya raia.

Mara ya mwwisho alikuwa Tanzania

Wakati wa tangazo hilo la kupinduliwa kwa serikali, Nkurunzinza alikuwa Tanzania kuhudhuria mkutano wa viongozi wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki uliotishwa na mwenyekiti wa jumuiya hiyo Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kuujadili mzozo huo wa Burundi.

Waandamanaji wakisherehekea kupinduliwa kwa utawala wa Nkurunziza
Waandamanaji wakisherehekea kupinduliwa kwa utawala wa NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Niyombare aliagiza viwanja vyote vya ndege na mipaka yote ya ardhini ya Burundi kufungwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito wa dharura kwa pande zote nchini Burundi kuonyesha utulivu na kujizuia kufuatia jaribio la mapinduzi ya serikali dhidi ya Rais Nkurunzinza.

Msemaji wa katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujarric amesema Ban amesisitiza haja kwa viongozi wote wa Burundi kudumisha amani na uthabiti katika taifa ambalo limekumbwa na matukio ya ghasia mbaya katika kipindi cha nyuma.

Marekani imewataka waburundi kuweka silaha chini kufuatia ripoti za kupinduliwa kwa serikali ya Nkurunzinza na msemaji wa ikulu ya Rais wa Marekani Josh Ernest amesema nchi yake inafuatilia matukio yanavyojiri Burundi kwa makini na wasiwasi.

Marekani imesema bado inamtambua Nkurunzinza kuwa kiongozi rasmi wa Burundi lakini inamshinikiza kuheshimu katiba ya taifa hilo na mikataba ya amani ilyofikiwa mwaka 2000 kwa kutogombea muhula wa tatu.

Marekani inatambua utawala wa Nkurunzinza

Hatma ya Nkurunzinza haijulikani baada ya ofisi ya Rais hapo jana kutangza anarejea nyumbani kutoka mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki nchini Tanzania na alitarajiwa kulihutubia taifa.

Baadhi ya wanajeshi wakisherehekea na raia kupinduliwa kwa serikali
Baadhi ya wanajeshi wakisherehekea na raia kupinduliwa kwa serikaliPicha: Reuters/G. Tomasevic

Lakini ndege yake haikuweza kutua mjini Bujumbura baada ya viwanja vya ndege kufungwa. Afisa wa ngazi ya juu wa Uganda ambaye hakutaka kutambuliwa kwasababu haruhusiwa kuongea na vyombo vya habari amesema ndege iliyokuwa ikimbeba Nkurunzinza ilitua katika uwanja wa Entebbe nchini Uganda lakini hakutaka kuthibitisha iwapo yuko nchini humo au alirejea Tanzania.

Kiasi ya watu 20 wameuawa tangu tarehe 25 mwezi uliopita baada ya Nkurunzinza kutangaza kuwania muhula wa tatu madarakani kinyume na katiba ya taifa hilo ambayo inaruhusu mihula miwili tu ya miaka mitano kila mmoja akidai muhula wake wa kwanza alichaguliwa na bunge na wala sio wananchi. Zaidi ya waburundi 50,000 wametorokea nchi jirani kufuatia ghasia za kabla ya uchaguzi unaotarajiwa mwezi ujao.

Mwandishi: Caro Robi/ap/afp/dpa

Mhariri: Sudi Mnette