1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu kwa wahamiaji kubadili njia ya kuingia Ulaya

10 Machi 2016

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi kuwa huenda wahamiaji wakatumia njia mbadala kufika Ulaya Kaskazini, baada ya kufungwa kwa njia yao inayopitia katika mataifa ya Balkan.

https://p.dw.com/p/1IAdk
Nchi za Balkan zimefunga mipaka yake na hivyo kuwazuwia wakimbizi waliojana nchini Ugiriki.
Nchi za Balkan zimefunga mipaka yake na hivyo kuwazuwia wakimbizi waliojana nchini Ugiriki.Picha: Getty Images/D. Kitwood

Njia kuu ya watu wanaojaribu kufika katika mataifa tajiri ya Ulaya Kaskazini imekuwa kuanzia Uturuki kupitia Ugiriki, na kuendelea kupitia Magharibi mwa eneo la Balkan. Lakini mataifa yaliyoko kwenye njia hiyo yalifunga mipaka yake wiki hii, na kuwaacha maelfu wakikwama na kuisababishia mgogoro mkubwa zaidi Ugiriki.

Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos, ameonya kuwa bila kuwepo na njia halali kuingia Ulaya, wahamiaji na wasafirishaji haramu wa watu watajaribu kutafuta njia nyingine mpya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema wasiwasi bado upo juu ya njia nyingine, akimaanisha hasa Libya na Italia, na kuongeza kuwa njia ya Balkan imefikia mwisho, na kwamba wanafanyakazi kuhakikisha hali inaendelea kuwa hivyo.

"Na matokeo ya mkutano wa kilele wa Jumatatu yametoa mchango mkubwa katika hilo. Tunataka idumu, ndiyo maana kuna mengi ya kufanya kabla ya mkutano ujao wa kilele. Siku za kuwaruhusu watu kuingia tu zimepita. Na hilo bila shaka ni la Ulaya nzima," alisema de Maiziere wakati akiwasili kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo yandani mjini Brussels.

Griechenland Mazedonien Flüchtlinge bei Idomeni
Wahamiaji wakikumbana na senyenge kwenye mpaka wa Macedonia na Ugiriki.Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Kauli ya Merkel, Tsipras

Kauli hiyo ya waziri de Maiziere inakinzana na msimamo wa bosi wake Kansela Angela Merkel, ambaye kwa pamoja na waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras, wamekosoa hatua ya kufunga mipaka iliyochukuliwa na Austria na mataifa ya Balkan, huku waziri mkuu Tsipras akionya kuwa Ulaya haitakuwa na mustakabali ikiwa hali itaendelea kuwa hivyo.

Umoja wa Ulaya unakabiliwa na mgogoro juu ya namna ya kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji usiyo kifani, ambao walifikia zaidi ya milioni moja mwaka 2015, wengi wao kutoka Syria, Afghanistan na Iraq, na wengi wao wakiwa na nia ya kufikia mataifa tajiri ya Ujerumani, Austria na yale ya Sandinavia.

Siku ya Jumatatu, umoja huo ulifikia makubaliano na Uturuki, yanayonuwia kudhibiti mmiminiko huo, ambapo Uturuki ilikubali kuwarejesha wahamiaji wataokataliwa kuignia Ulaya.

Lakini Kamishna mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussein, alisema siku ya Alhamisi kuwa makubaliano yanaweza kusababisha ufukuzaji jumla wa wahamiaji kutoka Ugiriki kwenda Uturuki, ambao ameutaja kuwa kinyume na sheria.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre, dpae.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo