HRW: Serikali ya Zimbawe yatumia 'corona' kuminya demokrasia
12 Februari 2021Wanaharakati Zimbabwe wanaishutumu serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa kwa kutumia suala la janga la corona kuwakandamiza wapinzani.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch jana Alhamisi, Zimbabwe ni kati ya nchi 23 za Afrika ambazo zinatumia janga la corona kuminya haki za raia.
Mwandishi wa habari Frank Chikowore, ni miongoni mwawaandishi wa habari waliokamatwa mwaka jana kwa kumhoji mwanasiasa wa upinzani na pia mwanaharakati ambaye alidaiwa kuteswa na maafisa wa usalama wakati wa vikwazo vya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
HRW: Sauti ya wanaharakati na wakosoaji yanyamazishwa?
"Hakukuwa na sababu yoyote kwa polisi kutukamata. Vyombo vya Habari vinakandamizwa nchini Zimbabwe. Nilidhani hali ingebadilika Mnangagwa alipochukua usukani 2017 lakini, inaonekana anafanya kilekile Mugabe alikuwa akifanya. Ninatarajia serikali ya Mnangagwa kufanya mengi zaidi kuhakikisha uhuru wa vyombo vya Habari unalindwa nchini.” Amesema Chikowore.
Soma pia: Zimbabwe yawalilia wafadhili na wakopeshaji wa kimataifa
Chikowore alienda katika zahanati kuwahoji wanaharakati watatu akiwemo Cecilia Chimbiri, walikokuwa wakitibiwa baada ya madai ya kuteswa. Chimbiri anaelezea masaibu yaliyomkuta ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa sababu ya kutaka ruzuku au malipo wakati nchi ilifungwa.
"Serikali zinazowajali raia wake zinachukua hatua madhubuti kuwasaidia. Lakini serikali yetu inaonekana kunyamaza kimya kuhusu hilo. KInachoendelea ni ufisadi wao, wizi kutoka kwa raia huku watu wakiendelea kuteseka. Na wananyamazisha kila sauti dhidi yao kwa kutumia janga la corona kama sababu. Si kwamba watu wanakiuka vikwazo vya kudhibiti covid-19 ndipo wanakukamata, bali hata ukiandika kwenye twitter kuhusu ukatili wa polisi." Amesema Chimbiri.
Ripoti ya Human Rights Watch inasema kukamatwa kwa wanaharakati hao watatu Pamoja na mwandishi wa Habari Chikowore, ni mfano tu wa namna serikali ya Zimbabwe inaminya uhuru wa Habari na wa watu kukusanyika.
HRW: janga la corona limeibua wimbi la ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.
Gerry Simpson ambaye ni mkurugenzi wa idara inayoshughulikia mizozo katika shirika la Human Rights Watch amesema janga la corona limeibua wimbi la ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.
Ameongeza kuwa visa vya Chikowore na wanaharakati wa chama cha MDC si pekee ambavyo ni vya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Mnangagwa chini ya kisingizio cha kujaribu kudhibiti virusi vya corona.
"Nchini Zimbabwe, tumerekodi namna ambavyo maafisa wa usalama wamewapiga waandishi wa habari, namna ambavyo kwa wiki tisa walimshikilia mwaandishi wa habari kwa sababu ya kuripoti kuhusu COVID-19 na jinsi mnamo mwezi Machi walipitisha sheria mpya inayotishia kumfunga mtu jela hadi miaka 20 akiripoti habari za uongo ikiwemo kuhusu COVID-19." Tumerekodi visa kama hivyo katika jumla ya nchi 23 barani Afrika". Amesema Simpson.
Elasto Mugwadi ambaye anaongoza tume ya haki za binadamu ya Zimbabwe amethibitisha kwamba tangu mwezi Machi mwaka jana nchi hiyo ilipotangaza vikwazo vya kudhibiti virusi vya corona, tume yake imepokea malalamiko kadhaa ya manyanyaso.
(DW, HRW)