HRW: Wasichana waliojifungua waacha shule Msumbiji
19 Februari 2024Hayo ni kulingana na ripoti iliyotolewa siku ya Jumatano na shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch.
Shirika la Human Rights Watch (HRW) limeelezea katika ripoti yake yenye kurasa 52 kuwa wasichana wenye watoto mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa na ukosefu wa usaidizi na malazi ambavyo hupelekea kuwa vigumu kutimiza majukumu yao ya shuleni na malezi ya watoto wao.
Elin Martinez, mtafiti mkuu wa haki za watoto katika shirika hilo la HRW amesema vikwazo hivi hupelekea wasichana wengi, ambao ni wajawazito au wenye watoto kuacha shule kabla ya kumaliza elimu yao ya msingi. kadhalika, ukosefu wa elimu ya bure husababisha wasichana wengi kutoka kaya maskini kuacha shule.
Soma pia:Uganda: Ruksa wasichana wadogo kutumia uzazi wa mpango
HRW imeitaka Msumbiji kupitisha kanuni zinazoweza kutekelezwa kisheria ili kuhakikisha haki ya wasichana ya kupata elimu wakati wa ujauzito na wanapojifungua, na pia kutoa elimu ya kina kuhusu elimu ya ngono na kuwepo pia vituo vya kulelea watoto.
Gharama kubwa ya elimu inahusisha ada, malipo ya uandikishaji, sare za shule na gharama zingine zisizo za moja kwa moja kama vile gharama ya usafiri.
Wachambuzi: Wasichana walitengwa kisheria
Mwaka 2003, serikali ya Msumbiji ilipitisha sheria ambayo iliwaamuru maafisa wa elimu kuwahamisha wasichana wajawazito na wenye watoto kwenye shule za usiku.
Agizo hili lilianisha kutengwa kwa wanafunzi hao katika mfumo rasmi wa elimu ya kitaifa, na hivyo kuwanyima wanafunzi hao haki ya kuendeleza elimu yao katika shule za msingi na sekondari.
Kutokana na shinikizo la mashirika ya kiraia nchini Msumbuji, serikali mnamo mwaka 2018 ilibatilisha hatua hiyo ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wajawazito na kina mama, lakini hadi leo hii walimu na hata wanafunzi hawana maelekezo yaliyo wazi kuhusu kulinda haki yao ya elimu.
Soma pia:Kiwango cha mimba za utotoni nchini Uganda bado kiko juu
Human Rights Watch inasema licha ya hatua hiyo ya serikali, Msumbiji bado inahitaji kukabiliana na vikwazo vikubwa vya kimfumo na kijamii wanavyokabiliana navyo wasichana ili kusalia shuleni.
Shirika hilo limesema pia kuwa liligundua kwamba baadhi ya walimu na mamlaka za shule waliwaelekeza wanafunzi katika shule za usiku kutokana na unyanyapaa, mazoea ya kibaguzi yaliyopo au mwongozo usio rasmi kutoka kwa maafisa wa elimu.
Msumbiji ina rekodi mbaya linapokuja suala la elimu ya wasichana. Inashikilia nafasi ya tano duniani kwa kushuhudia ndoa za utotoni huku kiwango cha mimba za utotoni pia kikiwa juu zaidi kuliko mataifa yote ya mashariki na kusini mwa Afrika.
Inaarifiwa kuwa angalau msichana mmoja kati ya kumi nchini Msumbiji hupata mtoto kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.