ICC: Bensouda hakufadhili kundi la waasi wa LRA
27 Septemba 2023Hii ni kufuatia taarifa ya mwanasheria mkuu wa Uganda kwamba wanachunguza madai hayo yaliyowasilishwa na wakili wa kundi la wahanga wa maovu ya kundi hilo miaka 20 iliyopita kaskazini mwa Uganda.
Kulingana na taarifa ya wakili wa wahanga hao iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari, mwanamke kwa jina Brigit Inder anayedaiwa kuwa msaidizi wa aliyekuwa mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda alikutana na kiongozi wa wakiganaji wa kundi la Lords resistance army LRA Joseph Kony mara kadhaa kati ya mwaka 2006 na 2016.
Katika kipindi hicho alimkabidhi vitita vya dola na pesa hizo Kony na kundi lake walizitumia kununua silaha kutoka kwa kundi la Janjaweed.
Inadaiwa kuwa taarifa hizo zilitolewa na wahanga wa maovu ya Kony waliochukuliwa mateka na kutumikishwa.
Soma pia:Marekani kujadiliana na ICC juu ya uhalifu dhidi ya Putin
Wakili wa kundi hilo anasema pesa hizo zilitolewa na mwendesha mashtaka Fatou Bensouda kupitia kwa msaidizi wake.
Hata hivyo, mwakilishi waICC kanda ya Afrika MasharikiMaria Mabinti amekanusha madai hayo alipohojiwa na DW
Uganda kufanyia uchunguzi madai hayo
Mwanamke huyo Brigit Inder alikuwa mkurugenzi wa shirika lijulikanalo kama WIGJ ambalo hujishughulisha na kupigania haki za wanawake lenye makao yake Netherlands ambako pia ndiko makao ya ICC inapatikana.
Baada ya kupokea madai ya kutolewa kwa pesa hizo kwa waasi wa LRA, mkuu wa sheria nchini Uganda Kiryowa Kiwanuka amelezea kuwa wataanzisha uchunguzi kuyathibitisha.
Amenukuliwa na shirika la AFP akiyaja kuwa madai ya kusikitisha na kuahidi kwamba hatua zitachukuliwa kuona ni kiwango gani Fatou Bensouda au ICC walihusika.
Soma pia:ICC yaanzisha uchunguzi mpya katika machafuko ya Sudan
Juhudi za kumpata mkuu wa sheria wa uganda kwa wakati hazikufua dafu.
Itakumbukwa kuwa kundi la LRA limewahangaisha kwa zaidi ya miaka 36 raia wa mataifa ya Uganda, sudan kusini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ya Jamhuri ya Afrika ya kati ambako inadaiwa ndiko aliko kwa sasa.