1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliofariki Gaza yaongezeka

1 Desemba 2023

Wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na kundi la wanamgambo la Hamas, imesema, karibu watu 178 wameuwawa Gaza kufikia jioni ya Ijumaa, baada ya kumalizika kwa muda wa siku saba wa kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/4ZhOz
Jahresrückblick 2023 Israel Hamas Gaza Vita vya Mashariki ya Kati
Mwanamke akimbeba mtoto akijaribu kukimbia mashambulizi Ukanda wa GazaPicha: Ali Jadallah/Andalou/picture alliance

Maafisa wanasema idadi ya watu waliojeruhiwa hiyo Ijumaa ni 589. DW haiwezi kuthibitisha kwa njia huru vifo katika vita hivyo vya Israel dhidi ya Hamas.

Wakati huo huo, jeshi la Israel IDF limesema limewalenga wanamgambo wa Hamas katika zaidi ya maeneo 200 tangu mapigano yalipoanza tena. Msemaji wa jeshi hilo Avichay Adraee ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwa Kiarabu kwamba, mashambulizi ya angani yamefanywa kaskazini na kusini mwa Gaza, yakiwemo maeneo ya Khan Younis na Rafah.

Nalo tawi la kijeshi la kundi la Hamas la Kikosi cha Qassam limesema limerusha maroketi kadhaa kuelekea Israel. Haya yanafanyika wakati Qatar ambayo ndiyo mpatanishi mkuu katika vita hivyo, ikisema inadhamiria kuendelea na juhudi pamoja na washirika wake kwa lengo la usitishwaji mwengine wa mapigano.

Siku zijazo ni za huzuni nyingi

Kwengineko Kamishena Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina UNRWA, Philippe Lazzarini amesema anatabiri "siku zijazo zenye huzuni kubwa."

Ukanda wa Gaza | Watu wayakimbia makaazi yao Khan Younis
Watu wakitoroka makwao baada ya Israel kuanza tena mashambuliziPicha: Yasser Qudih/Xinhua/picture alliance

Matamshi ya Lazzarini ni sawa na yale yaliyotolewa na mashirika mengine ya misaada yanayofanya shughuli zake Gaza kama Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji iliyosema kuanza tena kwa mapigano kutaiondoa hata ile afueni kidogo iliyokuwa imeletwa na kusitishwa kwa mapigano kwa muda na litakuwa ni janga kwa Wapalestina.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Palestina limesema zaidi ya malori elfu moja ya misaada yalifanikiwa kuingia Ukanda wa Gaza katika kipindi cha siku saba za mapigano kusitishwa.

Na hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa MarekaniAntony Blinken, amesema amefanya mazungumzo kuhusiana na Gaza ya baada ya mapigano na jinsi ya kuleta amani ya kudumu, alipokutana na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka mataifa ya Misri, Qatar, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu na Mamlaka ya Palestina huko Dubai kandoni mwa mkutano mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa.

Watu wawili wameuwawa Lebanon kutokana na mashambulizi ya Israel

Kulingana na Blinken wamejadiliana kuhusiana na haja ya kuongeza misaada ya kiutu Gaza na hatua ya kuachiwa kwa mateka zaidi wa Israel wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas, ambao wanachukuliwa na Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine kama kundi la kigaidi.

COP28 Mkutano wa Kilele wa mazingira Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken Picha: Saul Loeb/AP/picture alliance

Kwengineko machafuko yameanza tena katika mpaka wa Lebanon na Israel hapo jana Ijumaa, muda mfupi baada ya Israel kuanza tena operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza.

Chanzo cha usalama nchini Lebanon kimeliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba, makombora ya Israel yamevishambulia vijiji kadhaa na kuwauwa watu wawili. Hii ni baada ya wanamgambo kutoka kundi la hezbollah linaloungwa mkono na Iran kuyashambulia maeneo kadhaa ya Israel karibu na mpaka na Lebanon kabla machweo ya jua.

Vyanzo: DPA/ /dw/en/israel-hamas-war-gaza-death-toll-climbs-after-truce-ends/live-67601316