1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaanza tena Gaza baada ya mapatano kumalizika

1 Desemba 2023

Mapigano yameanza tena Gaza Ijumaa baada ya kumalizika kwa mapatano ya wiki moja kati ya Israel na Hamas, huku vifo vya kwanza viliripotiwa dakika chache baadaye, kulingana na maafisa wa afya katika eneo la Palestina.

https://p.dw.com/p/4ZeZH
Mashariki ya Kati| mwisho wa usitishaji mapigano | Mashambulizi ya angani Gaza
Israel imetangaza kuanza tena mashambulizi dhidi ya Gaza baada ya kumalizika kwa mapatano ya kusitisha mapigano.Picha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Jeshi la Israel limesema ndege za kivita "kwa sasa zinashambulia" maeneo ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, na waandishi wa habari wa AFP waliripoti mashambulizi ya anga kaskazini na kusini mwa eneo hilo.    

Marwan al-Hams, mkurugenzi wa hospitali ya Al-Najar huko Rafah kusini mwa Gaza, ambako Wapalestina wengi walikimbilia baada ya kuambiwa na Israel waondoke kaskazini mwa eneo hilo, amesema mashambulizi yameua takriban watu tisa katika mji huo, wakiwemo watoto wanne.

Kwingineko, watoto wawili waliuawa katika mashambulizi ya anga katika mji wa Gaza, alisema Fadel Naim, daktari katika hospitali ya Al-Ahli mjini humo.

Soma pia: Qatar, Misri zaendelea na mazungumzo ya kurefusha zaidi muda wa kusitisha mapigano

Chanzo kilicho karibu na Hamas kiliiambia AFP tawi la kijeshi la kundi hilo limepokea "amri ya kuanza tena mapigano" na "kuulinda Ukanda wa Gaza", huku mapigano makali yakiripotiwa katika maeneo ya mji wa Gaza.

Mapambano yalianza tena muda mfupi baada ya jeshi la Israel kusema kuwa limenasa roketi iliyorushwa kutoka Gaza, ikiwa ni ya kwanza kutoka eneo hilo tangu kombora liliporushwa dakika chache kabla ya kuanza kwa mapatano hayo Novemba 24.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema mapigano yameanza tena baada ya Hamas "kukiuka" makubaliano ya kusitisha mapigano.