Idadi ya watu duniani kufika bilioni 9.8 mwaka 2050
22 Juni 2017Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya shirika la kushughulikia idadi ya watu duniani katika Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa idadi ya hivi sasa ya watu duniani ya takriban bilioni 7.6 itaongezeka hadi watu bilioni 8.6 ifikapo mwaka 2030, bilioni 9.8 ifikapo 2050 na bilioni 11.2 ifikapo mwaka 2100.
Inaripotiwa kuwa karibu watu miliioni 83 wanazaliwa duniani kila mwaka, mkondo unaoonyesha ongezeko litakaloendelea hata kama viwango vya uzazi vitashuka kama inavyoshuhudiwa tangu miaka ya 1960.
John Wilmoth, mkurugenzi wa kitengo hicho cha idadi ya watu amesema ripoti hiyo imekusanya takwimu kutoka mataifa 233 au maeneo duniani na kuongeza idadi ya watu barani Afrika inakua kwa kiwango cha kasi na inatarajiwa nusu ya idadi ya watu duniani kati ya sasa hadi mwaka 2050, itarekodiwa katika bara hilo.
Kwa upande mwingine, idadi ya watu barani Ulaya itapungua katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebashiri kuwa kuanzia sasa hadi mwaka 2050 idadi ya watu itaongezeka hususan katika mataifa haya:
India, Nigeria, Congo, Pakistan, Ethiopia, Tanzania, Marekani,Uganda na Indonesia. Katika kipindi hicho hicho, idadi ya watu katika mataifa 26 ya Afrika itaongezeka karibu mara mbili. Nigeria ambayo hivi saa ni nchi ya saba duniani iliyo na watu wengi, inashuhudia ukuaji wa kasi wa idadi ya watu na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inakadiria itaipiku Marekani muda mfupi kabla ya kufikia nusu karne.
China hivi sasa ndiyo inaongoza kwa idadi ya watu ikiwa na watu bilioni 1.4, ikifuatiwa na India iliyo na watu bilioni 1.3 . Ifikapo 2024, India inatarajiwa kuipiku China. Ripoti hiyo inasema uzazi umepungua kwa takriban kila eneo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
Nchi kumi zilizo na idadi kubwa ya watu hivi sasa lakini zina viwango vya chini vya uzazi ni China, Marekani, Brazil, Urusi, Japan, Vietnam, Ujerumani, Iran, Thailand na Uingereza. Mbali na kupunguwa kwa ukuaji wa idadi ya watu, viwango hivyo vya chini vya uzazi vimesababisha kuongezeka kwa idadi ya wazee.
Idadi ya watu walio na umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea itaonegezeka kutoka watu milioni 962 hivi sasa hadi watu bilioni 2.1 ifikapo 2050. Robo ya idadi ya watu barani Ulaya tayari wana umri wa miaka 60 na juu.
Hata hivyo bado kuna pengo kubwa kati ya mataifa masikini na matajiri katika suala la usawa. Makadirio ya umri wa mtu kuishi katika mataifa tajiri inapindukia 80 huku watu wanaoishi Afrika wanatarajiwa kuishi hadi umri wa miaka 50.
Mwandishi: Caro Robi/ap/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman