IMF:Uchumi wa dunia kukabiliwa na kipindi kigumu zaidi, 2023
2 Januari 2023Mkurugenzi Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva alipokuwa akihojiwa jana na kituo cha habari cha CBS, alisema mwaka huu wa 2023 utakuwa mgumu kuliko mwaka uliyopita kwa sababu mihimili ya uchumi wa kimataifa ambayo ni Marekani, Umoja wa Ulaya na China, zinashuhudia kwa wakati mmoja kusuasua kwa shughuli zao.
Mwezi Oktoba, IMF ilipunguza matarajio yake kwa ukuaji wa uchumi wa kimataifa kwa mwaka 2023, kutokana na kuendelea kwa vita nchini Ukraine pamoja na shinikizo la mfumuko wa bei na viwango vikubwa vya riba vilivyobuniwa na Benki Kuu ya Marekani kwa lengo la kupunguza makali ya mfumuko wa bei.
Wakati huo huo, China imeachana na sera yake ya kukabiliana na maambukizi ya COVID19 na kuanza kufungua tena shughuli zake za kiuchumi, ingawa wanunuzi bado wamekuwa na tahadhari wakati maambukizi ya virusi vya corona yakiongezeka.
Soma zaidi: Mzozo wa Urusi na Ukraine waendelea kusababisha matatizo ya kiuchumi
Katika maoni yake ya kwanza mbele ya umma tangu mabadiliko hayo ya sera, Rais wa China Xi Jinping, katika hotuba yake ya Mwaka Mpya siku ya Jumamosi, alitoa wito wa juhudi zaidi na umoja wakati China ikiingia katika kile alichokiita "awamu mpya."
Ukuaji wa China wapungua mwaka 2022
Georgieva amesema kwa mara ya kwanza katika miaka 40, kuna uwezekano ukuaji wa China mnamo mwaka 2022 ulikuwa sawa au chini ya ukuaji wa kimataifa. Mkuu huyo wa IMF ameongeza kwamba kutokana na idadi kubwa ya maambukizo ya UVIKO19 yanayotarajiwa huko katika miezi ijayo, huenda uchumi wa China ukaathirika zaidi mwaka huu na hivyo kuzuia ukuaji wa kikanda na kimataifa.
Soma zaidi:IMF: Uchumi wa dunia unakuwa kwa kasi ndogo
Giorgieva ameendelea kwa kuonyesha umuhimu wa kuwa na mfumo imara wa usambazaji:
"Jinsi tulivyofanya kazi imesababisha utegemezi kupita kiasi katika usambazaji wa bidhaa kimataifa. Tulizingatia sana gharama. Kuhusu kufanya bidhaa za bei nafuu. Lakini Covid na vita isiyo na maana ya Urusi dhidi ya Ukraine vimetuonyesha kuwa hii haitoshi. Tunapaswa kufikiria usalama wa mfumo mzima wa usambazaji, na hiyo inamaanisha kuwa na vyanzo tofauti vya ununuzi wa bidhaa ambavyo hufanya uchumi kufanya kazi vizuri. "
Aidha kiongozi huyo wa shirika la fedha duniani amesema, uchumi wa Marekani unaonekana kuwa na ustahimilivu zaidi ambao unaweza kuisaidia kuepuka kudorora, tatizo ambalo linatarajiwa kuathiri kiasi cha theluthi moja ya uchumi wa dunia. Lakini hali hiyo ni hatari maana inaweza kukwamisha maendeleo yanayotakiwa kufanywa na Benki Kuu ya Marekani ili kurejesha mfumuko wa bei kwenye kiwango cha chini.