1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yapokea maombi ya kuitathmini Kenya

4 Oktoba 2024

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesema limepokea maombi kutoka serikali ya Kenya ya kufanya tathmini ya hali ya rushwa na ufanisi wa uendeshaji serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4lQIZ
Kenya, Rais William Samoei Ruto
Rais William Ruto wa Kenya.Picha: BRYAN R. SMITH/POOL/AFP via Getty Images

Msemaji wa IMF aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Kenya ilikuwa imeomba kufanyiwa tathmini ya hali ya uendeshaji serikali ambayo kwa kawaida huchunguza iwapo rushwa na mifumo dhaifu ya udhibiti inahujumu mapato ya taifa au kusababisha matatizo mengine ya kifedha.

Kenya imekuwa ikihangaika na deni kubwa la taifa ambalo limefikia viwango vya kutia wasiwasi.

Soma zaidi: Kenya yashuka zaidi katika nchi zisizoweza kukopesheka

Vile vile, uamuzi wake wa kuondoa mapendekezo ya kikodi ya mwaka ujao kutokana na shinikizo la umma umeweka kizingiti katika kupata msaada wa kifedha wa dola milioni 600 kutoka IMF. 

Chanzo kimoja kimesema tathmini itakayofanywa na IMF inalenga kuonesha dhamira njema ya serikali katika kurejesha imani na nidhamu katika ukusanyaji mapato na matumizi ya serikali.

Madai ya matumizi mabaya ya serikali na rushwa ndiyo masuala yanayotajwa kuwa chanzo cha maandamano makubwa yaliyoitikisa serikali ya Rais william ruto mnamo mwezi Juni.