1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, Urusi na China kwa pamoja zafanya luteka za kijeshi

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
21 Januari 2022

Majeshi ya majini ya China, Urusi na Iran yamefanya mazoezi ya kijeshi kaskazini mwa bahari ya Hindi. Nchi hizo zimearifu kwamba zinashiriki katika luteka hizo kwa lengo la kuimarisha usalama na ushirikiano baina yao. 

https://p.dw.com/p/45u8Q
Russland Ukraine | Das russische Militär führt auf der Krim massive Übungen durch
Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Msemaji wa mazoezi hayo kamanda wa kikosi cha wanamaji cha Iran, Mostafa Tajeddini ameeleza kuwa wanajeshi wa nchi hizo tatu walianza luteka hiyo mapema leo kwenye eneo la kilometa za mraba 17,000. Wanajeshi wa nchi hizo tatu watajaribu mbinu za kijeshi kadhaa ikiwa pamoja na kuokoa meli zinazowaka moto, kukomboa meli zilizotekwa na kupata mazoezi yanayoambatana na mapigano ya usiku. Kamanda Tojeddini amesisitiza umuhimu wa usalama na ushirikiano baina ya China, Urusi na Iran.

Mpango wa mazeozi ya pamoja kati ya nchi hizo ulianzishwa mnamo mwaka 2019 kwenye bahari za Hindi na Oman na hii ni mara ya tatu kwa nchi hizo kufanya mazoezi ya pamoja. Televisheni ya Iran imeripoti kwamba meli 11 za nchi  hiyo zinashiriki katika mazoezi hayo pamoja na manowari tatu za Urusi. Kikosi cha mapinduzi cha Iran pia kinashiriki kwa kutumia meli ndogo na helikopta.

Rais wa Iran Ibrahim Raisi
Rais wa Iran Ibrahim Raisi Picha: Iranian Presidency/AA/picture alliance

Tangu aingie madarakani mwaka uliopita rais wa Iran Ibrahim Raisi amekuwa anaimarisha ushirikiano na  Urusi na China. Waziri wa mambo ya nje wa Iran alifanya ziara nchini China wiki iliyopita na rais wa Iran mwenyewe alikutana na rais Vladimir Putin mjini Moscow wakati mazoezi hayo yanaendelea. Baada ya kurejea nyumbani rais wa Iran Ibrahim Raisi amesema kuendeleza uhushiano baina ya nchi yake na Urusi kutaimarisha usalama wa kikanda na wa dunia nzima kwa jumla.

Rais wa Iran Ibrahim Rais alipomtembelea rais wa Urusi Vladmir Putin, mjini Moscow
Rais wa Iran Ibrahim Rais alipomtembelea rais wa Urusi Vladmir Putin, mjini MoscowPicha: Präsident.ir

Kwa upande wake Urusi ilitangaza jana kwamba jeshi lake la wanamaji linaandaa mazoezi makubwa yatakayozihusisha meli zake zote za kijeshi katika mwezi huu na mwezi ujao na kwamba luteka hizo zitafanyika kwenye bahari ya Pasifiki na ile ya Atlantiki. Hatua hii ya Urusi inazingatiwa kuwa nchi hiyo inalenga kuonyesha nguvu zake za kijeshi wakati ambapo mvutano kati yake na nchi za Magharibi unaongezeka.

Hatua za kijeshi za Urusi zinafwatiliwa kwa karibu huku kukishuhudiwa mlundiko wa wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka wake na Ukraine hali inayozusha hofu ya kutokea vita lakini Urusi imekanusha vikali kuwa ina mpango wa kuivamia Ukraine.

Vyanzo: AP/RTRE