Iran yasema kuwa tayari kufufua makubaliano ya nyuklia
23 Septemba 2022Kauli hiyo aliitoa Rais wa Iran Ebrahim Rais siku ya Jumatano (21.09.2022) wakati akihutubia katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, na kusisitiza kuwa nchi yake ina nia thabiti ya kufikia makubaliano ya kuiepusha nchi yake kumiliki silaha ya nyuklia.
Rais amesema tayari Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano ya awali mnamo mwaka 2018, wakati huo ikiongozwa na Rais Donald Trump. Tangu mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979 yaliyomuondoa kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Mataifa ya Magharibi, Tehran imekuwa ikitofautiana na Marekani na kujinadi kama Taifa linalokabiliana na taifa hilo lenye nguvu.
Soma zaidi: Mkwamo kuhusu mkataba wa nyuklia wanufaisha pande husika
Suala la Iran kukabiliana na shinikizo kutoka Marekani limepelekea nchi hiyo kukuza mahusiano na Mataifa kama Urusi katika mpango wake wa kuboresha kombora la masafa marefu lakini pia kujaribu kusambaza fikra zake za kimapinduzi kwa Mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kwa kuwatumia wanamgambo wa madhehebu ya Shiia na washirika wengine.
Iran yakinzana na matakwa ya Marekani
Iran imekuwa ikisema mara kadhaa kuwa dhumuni lake ni kuwa na mpango wa nyuklia wa amani, lakini imekuwa ikitafsiriwa kama ishara ya kukinzana na Marekani na hata utaratibu wa dunia.
Baada ya Rais wa Marekani wakati huo, Donald Trump kujiondoa katita makubalino ya nyuklia na Iran ambayo yaliratibiwa na mtangulizi wake Barack Obama, Tehran iliachana na vizuizi vyote vilivyowekwa na makubaliano hayo juu ya urutubishaji wake wa nyuklia.
Juhudi za kuokoa makubaliano hayo sasa zimefikia katika hatua tete. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wameonya kuwa uwezekano wa kuokoa mpango huo unakaribia kutoweka.
Soma zaidi: Marekani haijaridhishwa na jawabu la Iran kuhusu nyuklia
Iwapo Iran itaafiki makubaliano mapya ya nyuklia, itatakiwa kupewa kama fidia, kulegezewa vikwazo vya kiuchumi, kuruhusiwa ufikiaji wa soko la kimataifa na hata upatikanaji wa sarafu za kigeni kama Dola za Marekani.
Ebrahim Rais amesisitiza kuwa kuna nia thabiti ya kutatua changamoto zote zilizopo kwenye makubaliano hayo ya nyuklia lakini amesema kilicho muhimu ni ´´utekelezaji wa ahadi.´´
Iran yakemea undumilakuwili wa Magharibi
Licha ya kutangaza nia yake ya kufikia makubaliano mapya, Ebrahim rais amekosoa uchunguzi mkali wa shughuli za nyuklia za Iran, wakati mipango ya nyuklia ya Mataifa mengine imesalia kuwa siri, hapa akiilenga Israel ambayo haijawahi kukiri au kukanusha kama kweli ina miliki silaha za nyuklia.
Israel ambayo inapinga kabisa makubaliano yoyote ya nyuklia, inaituhumu Iran kuficha azma kuu ya mpango wake wa nyuklia kwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa.
Soma zaidi: Makubaliano ya nyuklia ya Iran kufikiwa karibuni?
Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Marekani Joe Biden alisema kamwe hawatoruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia na kusisitiza kuwa nchi yake iko tayari kurejea kwenye makubaliano hayo ikiwa Iran itatekeleza vyema ahadi zake.
Iran imesema jana Alhamisi kuwa haijaona umuhimu wa kufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 bila dhamana ya Marekani kuwa safari hii haitajiondoa tena isipokuwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kusitisha uchunguzi wa mpango wa nyuklia wa Tehran, msimamo ambao maafisa wa Marekani wameutupilia mbali na kusema "sio wa busara".
AFPE