1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ireland Kaskazini yatimiza miaka 20 ya mkataba wa amani

10 Aprili 2018

Ireland ya Kaskazini leo Jumanne tarehe 10 inaadhimisha miaka 20 tangu kutiwa saini mkataba wa amani wa Ijumaa Kuu kati ya Uingereza na jamhuri ya Ireland  na Ireland ya Kaskazini.

https://p.dw.com/p/2vnl4
Robert Lebeck Ausstellung
Picha: Archiv Robert Lebeck

Viongozi walio fanikisha mkataba wa amani wa Ireland ya Kaskazini wamejumuika na watu wengine kuadhimisha kumbukumbu hiyo ya miaka 20 huko Belfast, Ireland ya Kaskazini. Kumbukumbu hiyo ni tangu kutiwa saini mkataba huo wa amani mnamo Ijumaa Kuu ya tarehe 10 mwezi Aprili mwaka 1998 kati ya Uingereza, serikali ya Jamhuri ya Ireland na pande zinazohusika katika Ireland ya Kaskazini za Waprotestanti na Wakatoliki

Mgogoro mbaya kuwahi kutokea ulikuwa ni baina ya Wakatoliki waliopigania Ireland Kaskazini iungane na Ireland na kuwa moja na Waprotestanti watiifu kwa Uingereza na waliotaka Ireland iendelee kuwa sehemu ya Uingereza.

Kulia: Waziri mkuu wa zamani wa Ireland Bertie Ahern Katikati: Seneta wa Marekani George Mitchell na Kushoto: Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blai
Kulia: Waziri mkuu wa zamani wa Ireland Bertie Ahern Katikati: Seneta wa Marekani George Mitchell na Kushoto: Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony BlairPicha: picture-alliance/dpa/D. Chung

Miongoni mwa waliohudhuria maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini Belfast ni waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, waziri mkuu wa zamani wa Ireland Bertie Ahern na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Makubaliano hayo ya amani yaliyosainiwa Aprili 10, mwaka 1998, kwa kiasi kikubwa yalimaliza rasmi miaka 30 au miongo mitatu ya mgogoro ambao ulisabbaisha vifo vya watu wapatao 3,000. Na katika miaka iliyofuata vikundi vingine vya kijeshi vilijiepusha na kukana vurugu kwa kuharibu silaha zao, na hatimae jeshi la Uingereza lilivunja kambi za vikundi hivyo pamoja na vituo vya ukaguzi vya Ireland ya Kaskazini.

Lakini miongo miwili baadae, mojawapo ya mafanikio makubwa ya mpango wa amani kati ya Waprotestanti na Wakatoliki wa kugawana madaraka katika Ireland ya Kaskazini uko mashakani. Utawala katika nchi hiyo ulianguka tangu Januari mwaka 2017 na jitihada za kuurudisha utawala huo zimeshindikana kutokana na tofauti zilizoibuka.Wakati huo huo Uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wa kufikia mapatano na chama kitiifu kwa Uingereza, Democratic Union, umechochea msimamo mkali miongoni mwa wazalendo. Waziri mkuu wa Uingereza May amefikia mapatano hayo ili kuiimarisha serikali yake yenye wingi mdogo bungeni mjini London..

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/W. Rattay

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha Sinn Fein Gerry Adams aliyeshiriki katika juhudi za kufikiwa mkataba wa Ijumaa Kuu amesema serikali ya bibi May imechukua hatua ya kuuhujumu mkataba huo . Adams amesema katika hotuba yake kwamba uamuzi wa serikali ya chama cha wahafidhina wa kujiondoa Umoja wa Ulaya mchakato unaojulikana kama Brexit ni tishio dhahiri la mkataba kwa ijumaa kuu.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony BlairPicha: Reuters/S. Rousseau

Tony Blair kiongozi wa zamani wa chama cha Labour ambaye aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza tangu mwaka wa 1997 hadi 2007, anapinga sana mchakato wa Brexit na anaunga mkono kwa dhati kurudiwa upya kura ya maoni juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman