1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Benny Gantz kutwishwa jukumu la kuunda serikali

16 Machi 2020

Benny Gantz Kiongozi wa chama cha buluu na nyeupe Israel na hasimu mkubwa wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anatarajiwa kupewa jukumu la kuunda serikali ya muungano baada ya kupata uungaji mkono mkubwa zaidi wa wabunge.

https://p.dw.com/p/3ZVUu
Benny Gantz - Blau Weiße Partei, Israel
Picha: Getty Images/G. Tibbon

Rais wa Israel Reuven Rivlin anatarajiwa kummpa rasmi Benny Gantz hii leo jukumu hilo la kujaribu kuunda serikali saa chache kabla ya bunge jipya la Israel Knesset kuapishwa.

Israel imekuwa bila serikali kwa zaidi ya miaka mitatu baada ya mkwamo wa kupatikana mshindi katika duru tatu za uchaguzi nchini humo. Badaa ya chaguzi hizo hakuna chama chochote kilichofanikiwa kupata wingi wa kura bungeni kuwezesha kuunda serikali.

Katika uchaguzi uliofanyika Machi 2 si upande wa Netanyahu wa mrengo wa kulia na vyama vya kidini au upande wa Gantz wa siasa za wastani za mrengo wa kushoto au vyama vya waraabu wa Israel uliweza kupata viti vya kutosha bungeni.

Hata hivyo Waziri Mkuu Benjamin Netayahu alidai kushinda uchaguzi huo baada ya chama chake cha Likud  kunyakua viti 36 katika bunge la Knesset lililo na wanachama 120 huku chama cha Gantz kikijinyakulia viti 33.

Hapo Jana upinzani ulikuja pamoja kumuunga mkono Gantz akiwemo Avigdor Liberman kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu pamoja na wabunge 15 wa mungano wa chama cha waarabu wa Israel.

Gantz akataa kushirikiana na Waziri Mkuu aliyeshitakiwa

Kombibild: Benny Gantz und Benjamin Netanjahu

Jana usiku Rais Rivlin aliwaita Gantz na Netanyahu kwa mkutano wa dharura katika makaazi yake mjini Jerusalem kujadili uwezekano huo wa kuunda serikali ya muungano. Baada ya mkutano huo Netanyahu na Gantz walitoa taarifa ya pamoja kukubaliana kuwa makundi ya wapatanishi wa vyama vyao yatakutana haraka iwezekanavyo kujadili hayo.

Aidha mazungumzo ya kuunda serikali yalikwama awali kufuatia Netanyahu kukataa kuachia nafasi ya Waziri Mkuu  na Gantz kukataa kuwa pamoja na Waziri Mkuu aliyeshitakiwa. 

Kesi ya Netanyahu inayohusiana na ufisadi inapaswa kusikilizwa siku ya Jumanne lakini iliahirishwa hadi May 24 baada ya mahakama kuwekwa katika hali ya tahadhari kama njia moja ya kuzuwiya kusambaa kwa virusi vya Corona.

Netanyahu ameshitakiwa kwa makosa ya kutoa hongo, udanganyigu na kuvunja uaminifu  katika visa vitatu vya rushwa baada ya kutoa msaada wa kisiasa ili kuangaziwa vituri na vyombo vya habari na kuwasaidia wafanya biashara tajiri kupata zawadi za kifedha.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Israel kuwa waziri Mkuu aliye madarakani anakabiliwa na mashitaka.

Chanzo: dpa/afp