Israel, Misri zaafiki misaada ya kiutu kuingia Gaza
19 Oktoba 2023Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi Jumatano usiku wakati akirejea Washington baada ya ziara takriban saa nane huko Israel. Biden amewaambia waandishi wa habari kwamba El-Sisi amekubali kufungua kivuko cha Rafah na kuruhusu malori yapatayo 20 yaliyosheheni misaada ya kibinadamu, inayopelekwa kwa watu wa Gaza ambao wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, maji, mafuta na bidhaa nyingine muhimu baada ya Israel kuuzingira ukanda huo na kuushambulia kwa makombora kwa muda wa siku 12.
Hata hivyo Biden hajatoa tarehe rasmi ya kufunguliwa kwa kivuko hicho lakini Msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby amesema hilo litafanywa katika siku zijazo baada ya kukamilisha ukarabati wa barabara zilizoharibiwa. Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema katika taarifa yake baada ya uamuzi wa baraza la mawaziri kwamba "kutokana na maombi ya Rais wa Marekani Joe Biden, Israel haitozuia usambazaji wa misaada ya kiutu kupitia Misri".
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura Martin Griffiths ameliambia hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kwamba ofisi hiyo inadhamiria kupeleka hadi malori 100 kwa siku ya misaada huko Gaza, ikiwa ndio kiwango cha kabla ya kuibuka kwa mzozo kati ya Israel na Hamas, ambalo linazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na baadhi ya mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.
Hali bado ni tete baada ya hospitali ya Al-Ahli al-Arabi huko Gaza kushambuliwa
Maafisa wa Palestina wanasema tukio hilo la kinyama lilisababisha vifo vya watu 471. Israel na Hamas wanaendelea kutupiana lawama dhidi ya shambulizi hilo. Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetangaza leo hii kuwa watawala wa Hamas walizidisha idadi ya vifo katika tukio la hospitali hiyo kama sehemu ya kampeni yao ya upotoshaji.
Maandamano yalizuka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel. Watu wenye hasira waliandamana pia katika nchi za Iran, Jordan, Lebanon, Tunisia na kwingineko kufuatia shambulizi la hospitali hiyo. Ubalozi wa Marekani mjini Beirut ulishambuliwa kwa vilipuzi na waandamanaji wenye hasira ambao walitawanywa na vikosi vya usalama.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amewasili leo hii mjini Tel-Aviv na tayari amekutana na Rais wa Israel Isaac Herzog na wote wamesisitiza umuhimu wa kuepuka kuongezeka kwa vurugu katika eneo hilo. Alipowasili Israel Sunak amesema:
"Nimefurahishwa sana kuwa hapa. Ni wakati muhimu. Ni muhimu kwangu kuweza kudhihirisha mshikamano wangu na watu wa Israel kufuatia shambulio la kutisha la kigaidi. Tunaratajia kuwa na mikutano yenye tija."
Soma:Olaf Scholz aapa kufanya kazi na Israel kupeleka msaada Gaza
Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo leo Alhamisi na Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly na kusisitiza kuwa kipaumbele kwa sasa ni kusitisha mapigano na kuzuia vita hivyo kutanuka zaidi. Kulingana na shirika la habari la Interfax, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ameonya kuwepo hatari ya mzozo wa Gaza kuwa wa kikanda, na kwamba Urusi inaendeleza mawasiliano na Uturuki kuhusu mzozo huo.
Hadi sasa mzozo huo umesababisha vifo vya WaIsrael 1,400 huku Wapalestina wasiopungua 3, 478 wakiuawa na watu zaidi ya milioni 2 wakiishi katika mazingira mabaya katika ukanda wa Gaza.