Israel yaapa kulipiza kisasi baada ya vijana 12 kuuawa
29 Julai 2024Netanyahu amesema nchi yake itajibu vikali shambulio hilo. Baadhi ya mataifa yameeleza wasiwasi wao kuhusu kutanuka kwa mzozo huo, huku baadhi yakijiandaa kuwaondoa raia wao kutoka kwenye eneo hilo.
Akiwa katika eneo hilo, Netanyahu amesema raia wote wa Israel na bila shaka watu walio wengi duniani wameshtushwa mno na mauaji hayo ya kutisha huku akisema kuwa Israel haiwezi kupuuza kitendo kilichosababisha vifo vya watoto 12 wa Israel na kwamba jibu lao litakuwa kali zaidi.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Majdal Shams wameandamana kupinga ziara ya Netanyahu eneo hilo baada ya mazishi ya mhanga wa mwisho leo hii yaliyowakusanya mamia ya watu. Wakazi wengi wa Majdal Shams walikataa kuchukua uraia wa Israel tangu iliponyakua eneo la milima ya Golan kutoka kwa Syria mnamo mwaka 1967.
Kauli ya Netanyahu na mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyosababisha vifo vya watu wawili kusini mwa Lebanon vimeongeza hali ya taharuki hadi kuvuruga safari za ndege katika uwanja wa kimataifa wa Beirut. Jumuiya ya kimataifa imetoa miito ya kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha mzozo huo unageuka kuwa vita vya kikanda.
Soma pia: Israel yaapa kujibu shambulizi la Milima ya Golan
Hata hivyo mataifa kadhaa yameelezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa uhasama kati ya Israel na kundi la Hezbollah. Wizara ya Mambo ya Nje ya Cyprus imesema hivi leo kuwa iko katika hali ya tahadhari na imejiandaa kuwaondoa raia wake kutoka Mashariki ya Kati ikiwa itahitajika na kama hali ya mvutano itaendelea kuongezeka.
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani amefanya mazungumzo na wenzake wa Israel, Israel Katz na wa Lebanon Abdallah Bou Habib na kuwataka kusitisha mapigano na wimbi la ghasia. Lakini serikali mjini Tel-Aviv imesema inalenga kuiadhibu Hezbollah na si kulitumbukiza eneo hilo katika vita kamili.
Gaza yaendelea kushambuliwa na Israel
Israel imeendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza hasa katika mji wa kusini wa Khan Younis . Pia, maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuondoka katika eneo lililotajwa kuwa salama katikati mwa Gaza baada ya kuamriwa na jeshi la Israel. Wapalestina wametaja kuchoshwa na hali hiyo kama anavyoelezea Samah Abu Toyma, aliyempoteza ndugu yake kufuatia mashambulizi ya leo Jumatatu:
"Mauaji haya hayakubaliki. Kila siku kunatokea mauaji katika mzunguuko kwenye eneo la Abu Hamid, na kila wakati ninapokwenda huko jambo hilohilo hutokea."
Soma pia: Israel yashambulia shule huko Gaza na kuuawa watu 30
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekuwa akikabiliwa na maandamano ya kila wiki ya Waisraeli wanaotaka kufikiwe makubaliano ya usitishwaji mapigano na kufanikisha kuachiliwa kwa zaidi ya mateka 100 ambao bado wanashikiliwa na Hamas huko Gaza.
Hata hivyo mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Marekani, Misri na Qatar yamekuwa yakisuasua na hadi sasa hayajaonyesha dalili zozote za kufanikiwa licha ya Washington kutaja mara kwa mara kuwa makubaliano yanakaribia.
(Vyanzo: DPAE, AP, RTRE, AFP)