Israel yadai kuwauwa viongozi sita wa Hamas
16 Oktoba 2023Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa leo na Jeshi la Israel (IDF) lililosema viongozi hao wenye vyeo vya juu waliouliwa ni pamoja na maafisa wa kisiasa na kijeshi.
Taarifa ya IDF imewataja pia viongozi wawili wa Hamas ambao waliuawa wiki iliyopita, akiwemo Waziri wa Uchumi wa Hamas, Jawad Abu Shamala, na Zakaria Abu Maamar, ambaye inasemekana alihusika na masuala ya mahusiano ya kimataifa.
Soma zaidi: Wapalestina 2,220 wameuawa katika mashambulizi ya Israel ukanda wa Gaza
UN: Takriban watu milioni moja watoroka makazi yao Gaza
Siku ya Jumapili, Israel iliendeleza usiku kucha mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa lengo la kulisambaratisha kundi la Hamas, lakini viongozi wengi wa kundi hilo linalozingatiwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kama la kigaidi, wanaishi nje ya nchi.
Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiongezeka kufanikisha hatua ya kupata njia salama katika kivuko cha Rafah, ili kupitisha misaada kuingia Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kuamuru kuzingirwa kwa ukanda huo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekanusha taarifa za usitishwaji mapigano na Hamas.