1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaishambulia tena Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani

17 Julai 2024

Jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya makumi ya watu, licha ya ukosoaji wa mshirika wake Marekani kuhusu ongezeko la vifo vya raia.

https://p.dw.com/p/4iPIp
Shule ya UNRWA iliyoshambuliwa katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat, Gaza
Shule ya UNRWA iliyoshambuliwa katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat, GazaPicha: Omar Ashtawy/APA/ZUMA/picture alliance

Mamlaka za Ukanda Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas zimesema kuwa makumi ya Wapalestina wameuawa usiku wa kuamkia leo katika mashambulizi matatu tofauti katika maeneo ya kusini na katikati mwa ukanda wa Gaza. Watu 17 wameripotiwa kuuawa katika shambulizi kwenye kituo cha mafuta huko Al-Mawasi kusini mwa Gaza.

Msemaji wa taasisi ya ulinzi wa raia huko Gaza Mahmud Bassal amesema mashambulizi hayo ya anga yamewaua takriban watu 44 na kuwajeruhi makumi ya wengine. Baadhi ya mashambulizi yameripotiwa pia katika maeneo yaliyotajwa kuwa "salama" kama katika shule ya Al- Razi katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat, katikati mwa Gaza.

Soma pia: Israel yaishambulia kwa mabomu Gaza licha ya ukosoaji wa vifo vya raia

Israel imethibitisha kuwa ilifanya mashambulizi mawili na imekuwa ikidai kuwa ni katika lengo la kulitokomeza kabisa kundi la Hamas. Hayo yanajiri wakati Israel ikikabiliwa na ukosoaji mpya wa mshirika wake Marekani ambayo imesema ongezeko la vifo vya raia huko Gaza halikubaliki.

Tuhuma za Hamas na kauli za Israel

Kiongozi mkuu wa Kundi la Hamas Ismail Hanniyeh ameishutumu Israel kwamba inazidisha mashambulizi yake ili kujaribu kukwamisha juhudi za upatanishi na kuzuia mpango wa usitishaji mapigano. Tuhuma ambazo zimekanushwa na serikali wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ambaye amesema:

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu Benjamin NetanyahuPicha: Nir Elias/Pool Photo/AP/picture alliance

" Hamas wanakabiliwa na shinikizo. Huu ndio wakati hasa wa kuongeza maradufu shinikizo hilo, ili kuwarejesha nyumbani mateka wote, walio hai na waliokufa, na pia tuweze kufikia malengo yote ya vita."

Hayo yakiarifiwa, makabiliano kati ya jeshi la Israel na wapiganaji wa Hezbollah wa Lebanon yamezidi kushika kasi katika eneo la mpakani. Kiongozi wa kundi hilo Sayyed Hassan Nasrallah amesema hivi leo kwamba Hezbollah itaendelea kushambulia ikiwa Israel itaendelea 'kuwalenga raia'.

Soma pia: Wizara ya Afya Gaza yasema watu 38,664 wameuawa tangu kuanza vita

Vyombo vya habari vya Lebanon vimesema kuwa watoto 3 ni miongoni mwa watu 5 waliouawa kufuatia shambulio la Israel. Tangu Oktoba mwaka jana, ghasia ghasia hizo zimesababisha vifo vya watu 511, wengi wao wakiwa wapiganaji lakini pia wakiwemo raia wasiopungua 104, hii ikiwa ni kulingana na takwimu zilizotolewa na shirika la habari la AFP.

Katika hatua nyingine, Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa taarifa hii leo na kusema kuwa Hamas iliongoza makundi mengine ya wanamgambo wa Kipalestina ili kuendesha shambulio la Oktoba 7 kusini mwa Israel, na kwamba kundi hilo liliendesha mamia ya vitendo vya uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kudhamiria, mauaji ya kukusudia, ukatili wa kijinsia, ubakaji, uporaji na utekaji nyara.

(Vyanzo: Mashirika)