1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yaendesha operesheni ndani ya hospitali Gaza

15 Novemba 2023

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limeendesha usiku wa Jumanne operesheni ndani ya hospitali kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza ya Al Shifa na kusema waliwalenga wapiganaji wa Hamas katika eneo maalum katika hospitali hiyo.

https://p.dw.com/p/4YpF2
Nahostkonflikt - Schifa-Krankenhaus
Raia wakiwa nje ya Hopitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza (10.11.2023)Picha: Khader Al Zanoun/AFP

Jeshi la Israel linadai kuwa kundi la Hamas linatumia mahandaki chini ya hospitali ya Al-Shifaa kama eneo la kamandi ya operesheni zao na sehemu pia wanakowashikilia mateka.

"IDF inaendesha operesheni ya ardhini huko Gaza ili kuwashinda Hamas na kuwaokoa mateka wetu. Israel inapambana na Hamas na sio raia wa Gaza. Katika wiki za hivi karibuni, IDF imeonya mara kwa mara kwamba kundi la Hamas linaendelea kuitumia al-Shifaa kwa malengo ya kijeshi. Kwa hivyo, hospitali hiyo inahatarisha hadhi yake ya kulindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, " amesema Daniel Hagari ambaye ni msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).

Lakini madai hayo ya jeshi la Israel yamekanushwa vikali na daktari wa hospitali ya Al-Shifaa Ahmed El Mokhalalati. Shirika la Msalaba mwekundu na Shirika la Afya Duniani (WHO) wametaja kuwa na wasiwasi mkubwa kufuatia harakati za kijeshi  za Israel katika hospitali hiyo.

Israels Armeesprecher Daniel Hagari
Daniel Hagari, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).Picha: Gil Cohen-Magen/AFP

WHO imesema pia kuwa hospitali 22 kati ya 36 sasa zimeacha kufanya kazi huko Gaza, huku hospitali 14 ambazo bado zinafanya kazi zikiwa hazina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa, hasa wale wanaohitaji uangalizi mkubwa.

Hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ameitolea wito Israel kujizuia na kukomesha pia mauaji ya wanawake na watoto. Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Catherine Russell amesema alishuhudia matukio ya kutisha wakati wa ziara yake huko Gaza huku akizitaka pande zote zinazohusika katika mzozo huo kusitisha mara moja vita hivyo.

Hospitali zasitisha shughuli zao huko Gaza

Umoja wa Mataifa umesema kutokana na uhaba wa mafuta, ni hospitali moja pekee kaskazini mwa Gaza ndio inayoendelea kuwapokea wagonjwa na kutoa huduma.

Nahostkonflikt - Schifa-Krankenhaus
Wagonjwa na raia wakiwa ndani ya hopitali ya al-Shifa huko Gaza (10.11.2023)Picha: Khader Al Zanoun/AFP

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza hii leo kuwa hospitali pekee ya Al-Ahli ambayo kwa sasa ina jumla ya wagonjwa 500, ndio pekee inayoendelea kutoa huduma kaskazini mwa Gaza lakini pia inakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu.

Soma pia: EU yalaani vitendo vya Hamas kuwatumia raia kama ngao

OCHA imesema hospitali nyingine huko Gaza zote zimesitisha shughuli zao kutokana na uhaba wa umeme, vifaa vya matibabu, hewa ya oksijeni, chakula na maji. Hali hiyo imechochewa pia na milipuko ya mabomu na mapigano katika maeneo yaliyo karibu na hospitali. Leo hii, lori la kwanza lililobeba mafuta limevuka mpaka na kuingia Gaza.

Israel imeapa kulitokomeza kundi la Hamas  ambalo liliwaua watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200 katika shambulio lao la Oktoba 7, lakini mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel tayari yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 11.000 huku wengine takriban 30,000 wakijeruhiwa, hayo ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa na Wizara ya Afya ya huko Gaza.