Israel yaitwanga Gaza kabla ya kura ya usitishaji vita UM
20 Februari 2024Mapigano yasiyokoma yaliodumu kwa miezi minne sasa yamesambaratisha sehemu kubwa ya eneo hilo la Wapalestina, na kuwasukuma watu milioni 2.2 kwenye ukingo wa njaa na robo tatu ya watu kuyakimbia makaazi yao, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
"Ni wangapi kati yetu wanapaswa kufa ... ili kukomesha uhalifu huu?" alisema Ahmad Moghrabi, daktari wa Kipalestina kusini mwa mji mkubwa wa Gaza, wa Khan Yunis. "Ubinadamu uko wapi?"
Madola makubwa yanayojaribu kutafuta njia ya kuondoka kwenye mzozo huo unaotishia kusambaa yanapanga kuwasilisha azimio katika Baraza la Usalama Jumanne, kushinikiza usitishaji vita, ambalo Marekani imeahidi tayari kulipigia kura ya turufu.
Baada ya kupambana kuja na msimamo wa pamoja, mataifa yote ya Umoja wa Ulaya isipokuwa Hungary, yalitoa wito jana wa kusitisha vita mara moja kwa sababu za kiutu.
Pia yameihimiza Israel kutouvamia mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, ambako Wapalestina karibu milioni 1.5 wanajihifadhi.
Mji huo ambao ndiyo wa mwisho usioguswa na majeshi ya ardhini ya Israel, ndiyo pia lango kuu la misaada inayohitajika sana kupitia nchi jirani ya Misri.
Mashambulizi ya Isrel dhidi ya mji huo yanatatiza operesheni za kiutu, huku ugavi wa chakula ukivurugwa na ufungaji wa mara kwa mara wa mpaka, kulingana na shirika la wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa, UNRWA.
Uhaba wa chakula na maji umewaacha watoto na wanawake kote katika ukanda huo wakikabiliwa na ongezeko kubwa la utapiamlo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto lilionya Jumatatu.
Mtoto mmoja kati ya sita kaskazini mwa Gaza sasa wana utapiamlo, UNICEF ilisema, hali ambayo inaelekea kuzidisha kiwango ambacho tayari hakivumiliki cha vifo vya watoto.
Soma pia: Kipi kitaishawishi Misri kufungua mipaka kwa Wapalestina
Licha ya wito wa mara kwa mara wa kuiepusha Rafah, Israel imetoa muda wa hadi kufikia mwezi wa Ramadhani kwa Hamas kuwaachilia mateka wanaondelea kushikiliwa vingine itaendelea na uvamizi wa ardhini.
"Ikiwa kufikia Ramadhani mateka hawatakuwa nyumbani, mapigano yataendelea kila mahali ikiwemo eneo la Rafah," mjumbe wa baraza la mawaziri la vita Benny Gantz alisema.
Mwezi huo mtukufu wa Kiislamu unatarajiwa kuanza Machi 10. Wapatanishi wa kimataifa wamekuwa wakihangaika kuepushamashambulizi hayo na mauaji yanayohofiwa ya raia wengi.
Rasimu mbili hasimu za kusitisha vita
Katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mapendekezo mawili yanayopingana ya kusitisha mapigano yametolewa.
Rasimu ya kwanza, iliyoandaliwa na Algeria, inadai kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa misingi ya kibinadamu na "kuachiliwa bila masharti kwa mateka wote".
Lilikumbana na upinzani wa haraka kutoka kwa mfadhili mkuu wa Israel, Marekani, ambayo iliwasilisha rasimu mbadala.
Andiko hilo, lililoonekana na AFP siku ya Jumatatu, linasisitiza "uungaji mkono wa usitishaji mapigano kwa muda Gaza kwa haraka iwezekanavyo".
Pia linaelezea wasiwasi wake kwa Rafah, likionya kwamba mashambulizi makubwa ya ardhini "yatasababisha madhara zaidi kwa raia" na uhamaji.
Kulingana na chanzo cha kidiplomasia, rasimu hii pia ina nafasi ndogo ya kupitishwa kama ilivyoandikwa, na ina hatari ya kupigiwa kura ya turufu na Urusi.
Shinikizo kwa Netanyahu kuwakomboa mateka
Wakati Marekani imeshinikiza makubaliano ya kusitisha vita kwa ajili ya kuwachiliwa mateka, mazungumzo ya wiki kadhaa yanayohusisha wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar yameshindwa kufikia makubaliano.
Hamas imetishia kujiondoa katika mazungumzo hadi pale msaada zaidi utakaporuhusiwa kuingia Gaza, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akikataa matakwa ya Hamas na kuyataja kama "ndoto."
Soma pia: Waziri wa Wapalestina aishutumu Israel kwa ubaguzi wa rangi
Alipinga vikali wito wa majadiliano kujumuisha kutambuliwa kwa taifa la Palestina. "Tunakataa kabisa hili," alisema katika taarifa ya video siku ya Jumatatu, akisema "itahatarisha uwepo wa taifa la Israeli."
Mwishoni mwa juma, waandamanaji wa Israel walijaribu kuzuia malori ya misaada katika mpaka wa Misri na Gaza ili kuongeza shinikizo la kuachiliwa kwa mateka.
Mjini Jerusalem, waandamanaji waliandamana hadi kwenye nyumba ya Netanyahu, wakimtuhumu kwa kuwatelekeza mateka.
"Hakuna njia nyingine ya kuwarudisha watu hawa bila makubaliano," alisema mwandamanaji Eli Osheroff.
Mateso ni mpaka lini?
Vita hivyo vilianza baada ya Hamas kufanya mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa tarehe 7 Oktoba ambayo yalisababisha takriban watu 1,160 kuuawa kusini mwa Israel, wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu za Israel.
Wanamgambo wa Hamas pia walichukua mateka wapatao 250 -- 130 kati yao wakiwa wamesalia Gaza, wakiwemo 30 wanaodhaniwa kuuawa, kulingana na Israel.
Kampeni ya kulipiza kisasi ya Israel imeua takriban watu 29,092, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na hesabu ya hivi karibuni ya wizara ya afya ya eneo hilo.
Kwa wiki kadhaa, Israel imejikita katika operesheni zake za kijeshi huko Khan Yunis, mji alikozaliwa kiongozi wa Hamas katika eneo la hilo, Yahya Sinwar, anayedaiwa kuwa mpangaji mkuu wa shambulio la Oktoba 7.
Mapema Jumanne, walioshuhudia walisema mashambulizi ya anga ya usiku na mapigano yaliilenga zaidi Khan Yunis na uapnde wa mashariki mwa mji wa Gaza.
Soma pia: Israel yakabiliwa na shinikizo jipya kutoka Marekani dhidi ya kuishambulia Rafah
"Makombora yanatuangukia. Ni kwa kiasi gani mwanadamu anaweza kukabiliana zaidi na hilo?" Alihoji Ayman Abu Shammali baada ya mkewe na binti yake kuuawa katika shambulio la Zawayda, katikati mwa Gaza.
"Watu wa kaskazini wanakufa kutokana na njaa wakati sisi hapa (tunakufa) kutokana na mabomu."
Kundi la wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru Jumatatu kuhusu dhulma za Israel dhidi ya wanawake na wasichana wa Kipalestina, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na unyanyasaji wa kingono.
Israel ilisema madai hayo ni "ya kuchukiza na hayana msingi".
Chanzo: AFP, AP, DPAE