Israel yakabiliwa na shinikizo dhidi ya kuishambulia Rafah
16 Februari 2024Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa, ataendelea na kile kilichoitwa "oparesheni kubwa" katika mji huo ili kupata ushindi kamili dhidi ya kundi la Hamas.
Ikulu ya White House imesema kuwa Rais Joe Biden amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu jana jioni, na kumuhimiza dhidi ya kufanya shambulio katika mji wa Rafah pasi na kuwa na mpango wa kuhakikisha usalama wa raia.
Licha ya wito huo wa Biden, Netanyahu amesema kuwa Israel haitakubali kile alichokiita "maagizo ya kimataifa" kuhusu mzozo kati ya nchi yake na kundi la Hamas.
Soma pia: Viongozi wa dunia waisihi Israel kuacha operesheni ya Rafah
Mamia kwa maelfu ya watu wamekimbia makaazi yao katika ukanda wa Gaza na kuelekea mjini Rafah wakitafuta hifadhi katika kambi za muda zilizoenea karibu na mpaka wa Misri.
Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, mji huo umehifadhi zaidi ya nusu ya wakaazi wa Gaza, huku watu hao wakirundikana katika eneo moja.
Huyu ni mmoja wa waliokimbilia Rafah, "Kuishambulia Rafah kutakuwa tatizo kubwa kwa sababu ndio sehemu pekee inayotuhifadhi. Watu hapa ni wakarimu sana. Maumivu yetu ni yao pia. Hatuhitaji chochote zaidi ya kinachoendelea na Rafah ndio sehemu salama tuliyo nayo.
Uingereza yaeleza wasiwasi juu ya hali ya kibinadamu mjini Rafah
Uingereza, Australia, Canada na New Zealand pia zimeitoa mwito Israel kutofanya mashambulizi ya ardhini katika mji huo wa Rafah.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, imeeleza kuwa kiongozi huyo alifanya mazungumzo kwa njia ya simu naNetanyahu na kuelezea wasiwasi wa nchi hiyo kuhusu jinsi hali ilivyo mjini Rafah na hali mbaya ya kibinadamu inayoweza kutokea iwapo Israel itaendelea na oparesheni yake ya kijeshi.
Kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, mashambulizi ya Israel tayari yamegharimu maisha ya watu 112 mapema leo Ijumaa.
Ama kwa upande mwengine, Israel imeripoti kifo cha mwanajeshi wake katika ukanda wa Gaza leo na kuongeza idadi ya askari wake waliouawa tangu ilipoanzisha oparesheni ya ardhini dhidi ya Hamas kufikia 233.
Soma pia: Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza 'yafika pazuri'
Wapatanishi kutoka Marekani, Qatar na Misri wamekusanyika mjini Cairo ili kusaka makubaliano ya kusitisha mapigano na kuhakikisha watu walioshikiliwa mateka na Hamas wanaachiliwa kwa mabadilishano ya kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anaamini kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yanawezekana kuafikiwa.
"Tunaamini lazima suala la kuachiliwa huru mateka lipewe kipaumbele, na kuwarudisha nyumbani kwa wapendwa wao," amesema Blinken.
Mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Marekani CIA Bill Burns jana alifanya ziara nchini Israel ambayo haikutangazwa kwa ajili ya mazungumzo na Netanyahu na mkuu wa shirika la kijasusi la Israel Mossad, David Barnea.