Israel yapambana vikali na Hamas ndani ya Gaza
31 Oktoba 2023Tukianzia ndani ya Gaza, ni kwamba vikosi vya Israel vinaendelea na mapambano makali na wanamgambo wa Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza, huku taarifa ya jeshi la Israel IDF ikisema kwamba wamewaua wapiganaji kadhaa wa Hamas katika kipindi cha saa chache zilizopita na kukamata bunduki na vilipuzi.
Taarifa hiyo imeongezea kuwa mapigano yalituama zaidi ndani ya mtandao mkubwa wa chini ya ardhi katika eneo lililozingirwa la Gaza, ambapo Israel inatafuta kulisukuma kundi la Hamas kuwaachia huru mateka na kuendeleza kampeni yake ya kulitokomeza kundi hilo la wanamgambo.
IDF ilianza oparesheni ya kupelekea vifaru ndani ya Gaza kuanzia usiku wa Ijumaa wakati mashambulizi ya angani upande wa Kaskazini yakiongezeka. Mkuu wa kamandi ya kusini ya jeshi la Israel Meja Jenerali Yaron Finkelman amesema kwamba, "tunaanzisha mashambulizi dhidi ya Hamas na mashirika ya kigaidi katika Ukanda wa Gaza. Lengo letu ni moja tu, ushindi!. Haijalishi mapigano ni ya muda gani, ni magumu kiasi gani, hakuna matokeo mengine zaidi ya ushindi".
Hayo yakiendelea, shirika la afya duniani WHO limeonya kwamba "janga la afya ya umma" linainyemelea Gaza, katikati mwa msongamano mkubwa, kuwahamisha watu kwa nguvu na uharibifu wa miundombinu.
Msemaji wa WHO Christian Lindmeier ameonya uwezekano wa kutokea vifo vingi vya raia ambavyo havihusiani moja kwa moja na mashambulizi ya Israel.
Tahadhari hiyo inatolewa wakati Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) Philippe Lazzarini akiueleza mkutano wa dharura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu kwamba janga la kibinadamu linalotokea mbele ya macho yao halivumiliki. Lazzarini alitaja idadi ya watoto waliouwa huko Gaza kufikia 3,000 katika kipindi cha wiki tatu.
Maafisa wa afya wa Gaza wamesema zaidi ya Wapalestina 8,300 wameuawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya angani katika eneo hilo linalotawaliwa na Hamas, katika hatua ya kujibu shambulizi la Hamas la Oktoba 7 lililowaua watu 1,400 nchini Israel na kuwachukua wengine zaidi ya 200 kama mateka.
Kando na yanayotokea Gaza lakini yakihusiana na mzozo huo, ni kwamba waasi wa Kihuthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran wamerusha ndege za Droni kuelekea Israel kujibu vita vyake dhidi ya Hamas.
Soma kuhusu: Waasi wa Huthi wanaoungwa mkono la Iran kwenda Saudi Arabia
Hapo awali, jeshi la Israel liliripoti "uvamizi mkali wa ndege" ambao uliingilia ving'ora vya tahadhari katika eneo la Eilat, ambao ni mji wa mapumziko kwenye Bahari Nyekundu. Lakini baadae msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alidai kwamba "hapakuwa na kitisho wala hatari katika mkoa huo."
Israel iliwatuhumu waasi wa Kihuthi kwa shambulio kama hilo la Droni siku ya Ijumaa, ambapo ndege yake iliweza kuingilia kati shambulio hilo lililokuwa limeelekzwa upande wa kusini wa Israel.