Mgombea wa Ukansela wa CDU Armin Lachet atakiwa aachie ngazi
27 Agosti 2021Wanachama wengi wa chama cha Armin Laschet cha Christian Democratic Union CDU, sasa wanajiweka kando na mgombea wao na wengine wanataka ajiuzulu. Alipochaguliwa kuwa mgombea wa kambi hiyo ya wahafidhina, chama cha CDU kilikuwa kinaongoza katika kura za maoni lakini hali imebadilika na sasa chama hicho kinarudi nyuma. Kulingana na utafiti wa maoni, mgombea ukansela kwa tiketi ya chama cha Social Democratic SPD, Olaf Scholz ambye kwa sasa ni waziri wa fedha wa Ujerumani yupo kidedea akifuatiwa na mgombea wa chama cha kijani Annalena Baerbock.
Hata ikiwa chama cha CDU kitashika nafasi ya pili au ya tatu hayo yatakuwa maafa kwa kambi ya wahafidhina. Mambo sasa ni mabaya zaidi kwa Armin Laschet ambaye ni waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia lenye watu wengi zaidi kuliko jimbo jingine lolote la Ujerumani. Waliokuwa wanamuunga mkono wanamtaka aachie ngazi.
Mwenyekiti wa chama ndugu cha CSU katika wilaya ya Nuremberg kwenye jimbo la Bavaria Andre Freud amesema mambo hayaendi vizuri kwa kambi ya wahafidhina na kwamba hakuna matumaini ya hali ya kambi hiyo kubadilika. Kampeni ya bwana Laschet imekuwa inaandamwa na mushkeli. Alinaswa kwenye camera akiwa anacheka kwenye eneo lililokumbwa na maafa ya mafuriko hivi karibuni. Na wala hakuwa la kujibu alipoulizwa juu ya mipango ya baadae. Na jimbo lake la North Rhine Westphalia linaongoza kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Mwenyekiti wa CSU wa mji wa Nuremberg bwana Freud amesema mgombea ukansela huyo wa kambi ya wahafidhina anazingatiwa kuwa mtu asiyekuwa na hisia sahihi. Mwenyekiti huyo amefafanua kwa kueleza kwamba hata ikiwa bwana Laschet hayuko hivyo, watu wengi wanamzingatia kuwa hivyo. Andre Freud amemtaka bwana Armin Laschet aachie ngazi.
Baadhi ya wanahcma wa kambi ya wahafidhina wanataka nafasi ya Laschet ichukuliwe na mwenyekiti wa chama cha CSU, Markus Söder ambaye ni Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani.
Vyanzo:/RTRE/https://p.dw.com/p/3zX9h