1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je! Mkutano wa EU-China utaivuta China upande wa Magharibi?

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
1 Aprili 2022

Umoja wa Ulaya unataka kuionya China kwa kuiunga mkono Urusi na pia unataka China itumie ushawishi wake kusitisha vita vya Ukraine. Pana shaka iwapo hilo litawezekana wakati wa mkutano kati ya pande hizo mbili.

https://p.dw.com/p/49KXu
Symbolbild EU - China
Picha: Jason Lee/REUTERS

Mkutano huo wa kilele kati ya pande hizo mbili unafanyika kwa njia ya video. China imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa vita nchini Ukraine, hata hivyo pana tofauti kuhusu sababu za vita hivyo kati ya pande mbili za hizo. China inaunga mkono matamko ya Urusi dhidi ya Jumuiya ya kijeshi ya NATO, huku Umoja wa Ulaya na nchi za Magharibi zikisimama kinyume kabisa na mtazamo huo wa China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang YiPicha: Li Xin/Xinhua/picture alliance

Kabla ya kuanza mkutano huo wa kilele, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi ameiambia Televisheni ya Phoenix kwamba uhusiano wa China na Urusi unaendelea kustawi na wala hautetereki. Kwa upande wake Rais wa China Xi Jinping katika tamko lake rasmi la mwezi uliopita alisema nchi yake inasimamia amani na inapinga vita.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wana nia ya kuutumia mkutano huo wa kilele kati yao na China kujadili vita vya Ukraine. Waziri Mkuu wa Finland Sanna Marin amesema kabla ya mazungumzo hayo kuanza kwamba, watahakikisha kuwa China inasimama katika upande sahihi wa historia.

Baraza la Ulaya katika taarifa yake limesema mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yamepania kuanzisha tena mazungumzo juu ya haki za binadamu katika mkutano huo na China na vilevile kujadili maeneo mengine ya masilahi ya pamoja kama vile kukabiliana na maswala ya mabadiliko ya hali ya hewa na janga linaloendelea la COVID-19.

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya
Viongozi wa nchi za Umoja wa UlayaPicha: Michel Euler/AP/picture alliance

Andrew Small, mtaalam wa mambo ya China katika taasisi ya Marekani ya Mfuko wa Marshall tawi la Ujerumani, ameelezea kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya watautumia mkutano huo kama fursa ya kuionya China. Naye Reinhard Buttikofer, mwanachama wa Chama cha Kijani cha nchini Ujerumani katika Bunge la Ulaya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni na mwenyekiti wa Ujumbe wa China wa Bunge la Ulaya amesema uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na China ni mgumu zaidi na wenye migogoro mingi kwa sasa kuliko ilivyokuwa kwa muda mrefu na hasa katika mwaka jana.

Buttikofer amesema China ilianzisha muungano mpya na rais wa Urusi Vladimir Putin mwanzoni mwa mwezi wa Februari na kimsingi imeiunga mkono Urusi katika uchokozi wake dhidi ya Ukraine. Amesema China inaelekeza lawama kwa Marekani na jumuiya ya NATO lakini haikosoi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Mjumbe huyo wa chama cha Kijani amesema wanataka kuidhihirishia China kwamba suala hili litakuwa na athari katika mustakabali wa uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya na hivyo inapaswa kuzingatia kuacha kuiunga mkono Urusi.

Kulia: Reinhard Buttikofer, Mbunge wa Chama cha Kijani katika Bunge la Ulaya na mwenyekiti wa Ujumbe wa China wa Bunge la Ulaya.
Kulia: Reinhard Buttikofer, Mbunge wa Chama cha Kijani katika Bunge la Ulaya na mwenyekiti wa Ujumbe wa China wa Bunge la Ulaya.Picha: AP

Je, mkutano huu wa kilele utaifanya China ibadilishe msimamo wake na kuanza kuegemea upande wa Magharibi?

Wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya na NATO wameionya China kwamba inaweza kukabiliwa na madhara kutoka kwa nchi za Magharibi ikiwa itaendelea kuiunga mkono Urfusi, Joris Teer, mchambuzi wa maswala ya yanayohusu China mjini The Hague ameeleza kuwa kwa sasa China inaelekeza nguvu zake katika kile inachokiona kuwa ni vitisho dhidi yake na Marekani ikiwa ni moja wapo ya vitisho hivyo.

Chanzo: https://p.dw.com/p/49EPH