Je, mzozo wa China na Taiwan kuongezeka baada ya uchaguzi?
16 Januari 2024Matokeo ya uchaguzi wa rais na wabunge wa Taiwan yalikuja kama habari mbaya kwa Beijing na kuna uwezekano yataziweka pande zote mbili katika uhusiano wa msuguano endelevu, wataalam waliiambia DW.
Jumamosi usiku, chama tawala cha Taiwan cha Democratic Progressive Party (DPP) kilipongeza mafanikio yake ya kushinda urais kwa mara ya tatu mfululizo. Hilo lilivunja rekodi kwa sababu hakuna chama chochote cha siasa kilichosalia madarakani kwa zaidi ya mihula miwili tangu kisiwa hicho kilipomchagua kiongozi wake wa kwanza mwaka 1996.
William Lai Ching-te, rais mteule ambaye muhula wake utaanza rasmi Mei 20, alisema katika hotuba yake ya ushindi kwamba Taiwan imechagua "kusimama upande wa demokrasia" kinyume na utawala wa kiimla.
Baadaye usiku huo huo, Ofisi ya Masuala ya Taiwan ya China ilipuuza ushindi wa DPP ikisema matokeo yake hayawezi kuwakilisha maoni ya umma wa Taiwan. Iliongeza kuwa chaguzi hizi hazitazuia "mwenendo usiozuilika wa kuunganishwa tena kwa nchi mama."
Beijing inaichukulia Taiwan kuwa sehemu yake. Chini ya utawala wa kiongozi wa China Xi Jinping katika muongo mmoja uliopita, Beijing imezidisha azma yake ya "kuungana" tena na kisiwa hicho kinachotawaliwa kidemokrasia.
Fikra za Beijing kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Taiwan
Kabla ya uchaguzi huo, China iliitaja kura hiyo kama chaguo kati ya "vita na amani" na kumshutumu Lai kama "mtu hatari anaetaka kujitenga" ambaye, akichaguliwa kuwa rais, atakuwa tishio kwa amani ya kikanda.
Licha ya maonyo hayo, Lai mwenye umri wa miaka 67 alipata takriban asilimia 40 ya kura katika kinyang'anyiro kikali cha wagombea watatu na Hou Yu-ih kutoka chama kikuu cha upinzani cha Kuomintang (KMT) na Ko Wen-je kutoka chama kipya cha Taiwan People's Party ( TPP).
"Hawafurahishwi [China] na Lai. Ni habari mbaya kwa sababu mtu ambaye hawakutaka ashinde kashinda," Lev Nachman, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Chengchi cha Taiwan, aliiambia DW.
Soma pia:Wafahamu wagombea wakuu watatu wa urais Taiwan
Lakini "kuna jambo jema kwenye mtazamo wa PRC," alisema Nachman, akimaanisha China kwa ufupisho wa jina lake rasmi, Jamhuri ya Watu wa China. Alibainisha kwamba, kwa Lai kutopata asilimia 50 ya kura, ilimaanisha: "Asilimia kubwa zaidi ya watu hawakuipigia kura DPP au Lai. Hilo ni jambo kubwa."
Wakati huo huo, mtaalamu mwingine aliamini kwamba ushindi wa DPP ulikuwa "ndani ya matarajio ya China," hata kama kulikuwa na nia ya kuona uongozi wa Taiwan ukihamia vyama vya upinzani vinavyotaka mazungumzo zaidi na maelewano na Beijing.
Chang Wu-ueh, mtaalam wa uhusiano wa eneo la ujia wa bahari kutoka Chuo Kikuu cha Tamkang, aliiambia DW kwamba maafisa wengi wa China walitabiri matokeo hayo na walikuwa wakijiandaa kwa majibu yanayoweza kutokea.
"Hatua za kabla ya uchaguzi za vitisho vya kijeshi na shinikizo la kiuchumi zina uwezekano mkubwa wa kuongezwa katika zama za baada ya uchaguzi," Chang alisema.
Hakuna mabadiliko makubwa katika uhusiano
Taiwan, iliyoko umbali wa maili 100 kutoka China kuvuka Mlango-Bahari wa Taiwan, inaweza kuwa mojawapo ya maeneo yenye hatari kubwa zaidi ya kuibuka uhasama duniani. Katika miaka minane iliyopita ya utawala wa DPP, mazungumzo rasmi kati ya pande hizo mbili yamesitishwa.
Wakati Lai akitarajiwa kuchukuwa madaraka, Washington na nchi nyingine za kidemokrasia za Magharibi zinafuatilia kwa karibu jinsi sera yake ya China inaweza kubadilisha uhusiano wa eneo hilo ambao tayari umeyumba.
"Sidhani kutakuwa na vita, lakini nadhani PRC itaendelea kutopokea simu," alisema msomi Nachman, na kuongeza kuwa "mahusiano ya uhasama zaidi" yanatarajiwa kudorora na kwamba Lai hana uwezekano mkubwa kubadilisha hali ilivyo.
Chong Ja Ian, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore, aliiambia DW kwamba wakati Xi Jinping hajaridhika na matokeo na anataka kuongeza shinikizo kwa Taiwan, "anaweza kuwa na wasiwasi juu ya kuongezeka kwa mzozo kufikia viwango visivyoweza kudhibitiwa wakati ambapo uchumi wa China upo dhaifu zaidi."
Wakati wa hotuba ya jana, Lai aliahidi kuchukua hatua kwa mujibu wa katiba za "Jamhuri ya China," jina rasmi la Taiwan, kwa namna ambayo "itadumisha hali iliyopo."
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisisitiza azma ya "kudumisha amani na utulivu katika eneo Ujia wa Bahari " katika taarifa ya pongezi kwa Taiwan. Pia aliahidi kuendeleza "uhusiano wao usio rasmi wa muda mrefu."
Chang aliiambia DW kuwa mustakabali wa uhusiano wa Taiwan na China unaweza kutegemea uhusiano wa Pasifiki kati ya Marekani na China.
Soma pia: Jeshi la China liko tayari kuvunja njama za Taiwan kujitenga
"Maadamu uhusiano wa Marekani na China ni mzuri na tofauti zinaweza kudhibitiwa, Beijing inaamini kuwa uhusiano mkubwa wa Taiwan-Marekani-China unazidi ule mdogo wa China na Taiwan," alisema.
Mvutano katika Mlango-Bahari wa Taiwan ni chanzo cha mara kwa mara cha msuguano kati ya Beijing na Washington. Marekani, ambayo inaridhia sera ya China Moja ambayo ilitambua uhuru wa PRC pekee, imekuwa ikionyesha uungaji mkono kwa Taiwan kwa mauzo ya silaha na mabadilishano kati ya nchi mbili kwa kiwango kisicho rasmi.
Kwa mujibu wa ubalozi wa Marekani mjini Taipei, maafisa wawili waandamizi wa zamani wa Marekani watawasili Taiwan siku ya Jumapili kwa mazungumzo ya baada ya uchaguzi na kusisitiza "nia ya muda mrefu" ya serikali ya Marekani katika kutafuta amani katika Mlango wa bahari wa Taiwan.
Mtihani wa kweli kwa utawala unaofuata wa Taiwan
Hata hivyo, wataalamu wanaamini kuwa bunge jipya litakuwa mtihani mkubwa wa uongozi wa Lai, ikizingatiwa kuwa hakuna chama chochote cha kisiasa ambacho kimepata wingi wa kura katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Chong, profesa wa siasa nchini Singapore, aliieleza DW: "Rais asiye na wingi wa wabunge atalazimika kushughulikia ajenda zake za utungaji sheria, jambo ambalo linaweza kuathiri sera za kigeni."
Katika bunge la Taiwan lenye viti 113, DPP alipoteza viti 11 katika uchaguzi uliomalizika, na kutoa wingi kwa KMT, ambacho kilipata viti 52. Chama cha TPP, chenye viti 8 pekee, kinatazamiwa kuwa chama muhimu cha wachache, wakati vyama vikuu viwili vikipigania muungano.
Soma pia: Taiwan yaitaka China kugawana majukumu ili kudumisha amani
Hali kama hiyo, ambapo chama tawala kilishindwa kupata wengi, ilitokea mwaka wa 2000 wakati Rais wa zamani Chen Shui-bian wa DPP alipochaguliwa nchini Taiwan.
Profesa Chong alisema, wakati huo "kadiri Chen alivyozidi kuvunjika moyo," alianza kuunda sera yake ya Taiwan na China isiyo na hatari kubwa, ikiwa pamoja na sera yake ya "Nchi Moja kwa Kila Upande" ambayo ilionyesha kuwa China na Taiwan ni nchi mbili tofauti.
Ingawa tabia ya Lai inaonekana tofauti na ya Chen, Chong alisisitiza, "hakuna anayejua kwa wakati huu" jinsi kiongozi mpya anaweza kukabiliana na shinikizo kali wakati anasimama kwenye nafasi ya juu.