1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Je, Thailand inaweza kuiunganisha ASEAN kushinikiza Myanmar?

20 Desemba 2024

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Myanmar vimezidi kuwa vikali katika mwaka uliopita, huku waasi wa jamii za wachache wa kikabila wakitwaa maeneo makubwa kutoka utawala wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/4oRUB
Mzozo wa Myanmar
Mamilioni ya raia wa Myanmar wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo huo wa umwagaji damu na uchumi wa nchi hiyo uko katika hali mbaya.Picha: Kokang online media via AP/picture alliance

Wiki hii, Thailand imeandaa mikutano miwili ya kikanda kwa lengo la kushughulikia mgogoro wa kisiasa na usalama nchini Myanmar.

Mkutano wa kwanza ulihusisha utawala wa kijeshi wa Myanmar na majirani zake, ikiwa ni pamoja na China, Bangladesh, Laos, na India, wakati wa pili ulijumuisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) yenye wanachama 10.

Soma pia: Myanmar yaelezea maendeleo yaliyofikiwa kuelekea uchaguzi wa mwakani

Nchi zote jirani zilieleza kuwa ushirikiano wa moja kwa moja na mazungumzo na Myanmar ni "muhimu" na "lazima," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Thailand, Nikorndej Balankura, alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Bangkok.

Amnesty International yataka wanajeshi Myanmar wafikishwe ICC

"Waliona umuhimu wa kukutana mara kwa mara," Balankura aliongeza. "Na wanashiriki uelewa sawa, zaidi ya nchi zingine, kwa sababu wao ni majirani wanaoathiriwa moja kwa moja na hali ya Myanmar."

Mazungumzo yamehukumiwa kufeli?

Waziri wa mambo ya nje wa Myanmar Alhamisi aliwafahamisha washiriki kuhusu mwelekeo wa ramani ya kisiasa ya utawala wa kijeshi na mipango ya kufanikisha uchaguzi. Wakosoaji wamepinga mipango hiyo ya uchaguzi wakidai ni danganya toto.

David Scott Mathieson, mchambuzi huru anayeshughulikia migogoro na masuala ya haki za binadamu nchini Myanmar, alisema mazungumzo hayo hayawezi kuleta matokeo yoyote.

"Labda kama jeshi la Myanmar lina na nia ya dhati ya amani, mazungumzo haya hayatakuwa na tija. Huwezi kufanya diplomasia yoyote kuhusu Myanmar bila kuelewa wazi kwamba jeshi ndilo chanzo cha matatizo yote," aliiambia DW.

Soma pia: Mamlaka ya kijeshi nchini Myanmar yasisitiza kufanyika uchaguzi

Mathieson alisisitiza kuwa madai ya utawala wa kijeshi kuhusu kufanya uchaguzi hayapaswi kuchukuliwa kwa uzito.

"Hakuna mtu anayepaswa kuyachukulia madai haya kwa uzito. Huu ni mtego wa diplomasia. Ikiwa mpatanishi yeyote atachukua maandalizi ya uchaguzi kwa uzito, watakuwa wameihukumu nchi hiyo kuendelea na mgogoro kwa muda mrefu," alisisitiza.

Papa Francis ziarani Myanmar

ASEAN iliiambia nini junta ya Myanmar?

Thailand ilisema ilikuwa imewasilisha kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar kwamba wanachama wa ASEAN wangependelea uchaguzi uwe wa huru na wa haki.

"Ikiwa kuna uchaguzi, ASEAN itataka mchakato shirikishi ambao utahusisha wadau wote," Waziri wa Mambo ya Nje wa Thailand, Maris Sangiampongsa, alisema katika mahojiano ya kundi mjini Bangkok baada ya mikutano na wenzake wa ASEAN na wanadiplomasia waandamizi.

Kundi hilo bado linangoja maelezo ya uchaguzi kutoka upande wa Myanmar, maafisa wa Thailand walisema.

"Nchi jirani zilisema tunaiunga mkono Myanmar katika kutafuta suluhisho lakini uchaguzi lazima uwe shirikishi kwa wadau mbalimbali nchini humo," Maris alisema, akisisitiza kuwa majirani wa Myanmar watashauri, lakini hawataingilia moja kwa moja.

Mateso yasio na mfano wanayopitia Warohingya.

Hali ya sasa ya Myanmar ni ipi?

Myanmar imekuwa katika hali ya misukosuko ya kisiasa tangu jeshi lilipoipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia mnamo Februari 2021.

Mapinduzi hayo yalisababisha maandamano makubwa, ambayo yaliibuka kuwa upinzani mkubwa dhidi ya utawala wa kijeshi, hasa katika maeneo yanayotawaliwa na wachache wa kikabila.

Soma pia: Myanmar yafanya mgomo baridi katika kumbukumbu ya mapinduzi

Wanaopinga utawala wa kijeshi wameunda miungano inayojumuisha vikundi vya kikabila na vikosi vya ulinzi vinavyoongozwa na raia.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinakadiriwa kusababisha vifo vya zaidi ya raia 5,000 tangu 2021.

Mamilioni ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao, na uchumi wa nchi umedorora kabisa.

Mgogoro nchini humo umeongezeka zaidi katika mwaka uliopita, huku waasi wa jamii za wachache wa kikabila wakitwaa maeneo makubwa kutoka kwa utawala wa kijeshi, hasa karibu na mpaka wa China.

Elimu kwa Warohingya bado kitendawili

Je, Thailand inaweza kuwa na ushawishi?

Thailand na Myanmar zina historia ya karibu lakini yenye changamoto. Zote zinashirikiana kiutamaduni na kidini, pamoja na mpaka wa ardhini wa kilomita 2,400.

Tangu mapinduzi ya Februari 2021, raia wengi wa Myanmar wamekimbilia Thailand kutafuta maisha bora.

Thailand kwa sasa ina wakazi wa Myanmar wapatao milioni 2.

Pravit Rojanaphruk, mwandishi wa habari mkongwe na mchambuzi wa kisiasa, alisema kuwa Thailand ni nchi iliyoathirika zaidi na vita vya wenyewe kwa wenyewe na ukosefu wa utulivu nchini Myanmar.

"Bangkok itahitaji kujihusisha zaidi na kuwa na msimamo thabiti, sio tu kuhusu mgogoro wa kibinadamu bali pia kusaidia kuirudisha Myanmar katika njia ya amani na demokrasia," alisisitiza.