1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Fahamu mgawanyo wa Baraza jipya la mawaziri Afrika Kusini

Bakari Ubena Hairsine Kate
2 Julai 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitangaza siku ya Jumapili baraza lake jipya la mawaziri lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu- na kulazimika kugawana wizara na washirika wake.

https://p.dw.com/p/4hma2
Afrika Kusini | Cyril Ramaphosa akisalimiana na  John Steenhuisen wa chama cha DA
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (kulia) akisalimiana na Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance (DA), John SteenhuisenPicha: South African GCIS/AP/picture alliance

Hatua ya  Ramaphosa  inajiri baada ya chama chake cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wa viti buungeni, washirika wa ANC waliopo kwenye serikali ya mseto walikubaliana jinsi ya kugawana nafasi za mawaziri 32.

Kati ya vyama 11 vilivyopo katika serikali hiyo ya umoja wa kitaifa nchini Afrika Kusini, saba tu ndivyo vinawakilishwa katika baraza la mawaziri. Chama cha ANC kimeshikilia nyadhifa 20 katika baraza la mawaziri, zikiwemo wizara muhimu za ofisi ya rais, fedha, ulinzi, sheria, usalama na mambo ya nje.

Kuiweka wizara ya mambo ya nje chini ya mamlaka ya ANC huenda kukashuhudia serikali ya Afrika Kusini ikiendelea kuwaunga mkono Wapalestina na ukosoaji wake mkubwa wa harakati za Israel katika ukanda wa Gaza.

Watu wakiiangalia bendera ya Afrika Kusini
Watu wakiiangalia bendera ya Afrika KusiniPicha: UPI Photo/IMAGO

Kealeboga Maphunye, profesa wa siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini anasema rais Ramaphosa na chama chake cha ANC wametumia akili na busara kwa kusalia na wizara nyingi muhimu na zenye nguvu.

Soma pia: Rais Ramaphosa hatimaye ateua baraza jipya la mawaziri

Chama cha Democratic Alliance (DA), ambacho ni cha pili kwa ukubwa katika muungano huo, kimeambulia nafasi sita za mawaziri. Wiki iliyopita, ANC ilivunja ahadi yake ya kukipa DA wizara ya biashara na viwanda, jambo lilikwamisha kidogo mazungumzo. Badala yake, DA wamepewa wizara ya kilimo, elimu, mawasiliano, mambo ya ndani, mazingira na kazi za umma.

Wizara zingine sita ziligawanywa kati ya vyama vidogo. Chama cha Inkatha Freedom Party (IPF) kilipata wizara mbili huku vyama vya Freedom Front Plus, Good Patriotic Alliance na Pan Africanist Congress of Azania, kila chama kikipata wizara moja.

Je, mgao huo ulikuwa wa haki na unaangaliwaje na wafanyabiashara?

Kwa wizara sita pekee walizopata, Chama cha DA kimejikuta na sehemu ndogo ya wizara ikilinganishwa na asilimia 22 ya kura ilizopata katika uchaguzi. Hayo yameelezwa na Martin Plaut, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Mafunzo ya Jumuiya ya Madola, katika Chuo Kikuu cha London. Bwana Plaut amesema DA imepata nyadhifa ambazo anadhani zitakisaidia chama hicho kwa kuwa elimu na kilimo ni muhimu kwa uendeshaji wa nchi.

Sarafu ya Afrika Kusini ya randi
Sarafu ya Afrika Kusini ya randiPicha: Janusz Pienkowski/Zoonar/picture alliance

Thamani ya sarafu ya Afrika Kusini ya randi, iliongezeka kidogo Jumatatu asubuhi, na kuendelea kupanda kwa muda wa wiki moja mara baada ya tangazo la Ramaphosa ambalo kwa hakika lilihitimisha kipindi cha wiki kadhaa za mashaka kwenye masoko.

Soma pia: Ramaphosa atangaza baraza jipya la mawaziri

Lukmile Mondi, mhadhiri mkuu katika Shule ya Uchumi na Fedha katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand (WITS) nchini  Afrika Kusini amesema jamii ya wafanyabiashara inathamini mno utulivu hasa kwa kushuhudia kuwa Waziri wa Fedha Enoch Godongwana amesalia katika wadhifa wake.

" Nadhani baraza hilo la mawaziri litawavutia wawekezaji. Kama tunavyojua, wizara ya  fedha haikubadilisha uongozi. Pili, tunachojua pia ni kwamba mwelekeo wa kisera kuhusiana na mageuzi, mfano mageuzi ya kimuundo ambayo sote tumekuwa tukiyataka, hasa katika sekta ya nishati, yote yanaweza kutekelezwa, ikizingatiwa kwamba ANC na DA wote wanakubaliana na hilo. Hata hivyo, nadhani ni jambo la kutia moyo na la manufaa kwa biashara."

Soma pia: Wizara 12 zachukuliwa na vyama vya upinzani Afrika Kusini

Kabla ya uchaguzi, Baraza la Mawaziri la Ramaphosa lilijumuisha mawaziri 30 na sasa wamekua 32. Baadhi ya wizara sasa zina manaibu waziri wawili, na hivyo kuongeza idadi yao hadi kufikia 43. Watendaji wakuu wa serikali ambao ni pamoja na rais, makamu wa rais, mawaziri na manaibu wao sasa wanafikia jumla ya watu 77.

Katika hotuba yake wakati wa kutangaza baraza lake la mawaziri, rais Cyril Ramaphosa alitaja kuwa na nia ya kupunguza idadi hiyo lakini badala yake imeongezeka, akisisitiza kuwa waliona ni muhimu kutenganisha wizara fulani ili kuhakikisha masuala muhimu yanashughulikiwa kikamilifu.

(DW)