Juhudi mpya zaanzishwa ili kusitisha mapigano Gaza
22 Februari 2024Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema watu 94 wameuawa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, na hivyo idadi jumla ya vifo ikifikia watu 29,410 tangu kuanza kwa mzozo huu kati ya Israel na Hamas Oktoba 7, 2023.
Mapema leo asubuhi watu watatu wenye silaha walifyatua risasi kwenye barabara iliyo karibu na kituo cha ukaguzi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, na kuua Muisraeli mmoja na kuwajeruhi wengine wanane. Washambuliaji wawili waliuawa na mmoja alikamatwa na sasa anashikiliwa na polisi.
Soma pia: Shirika la mpango wa chakula duniani WFP lasitisha ugawaji chakula kaskazini mwa Gaza
Mjumbe wa Baraza la Vita la Israel Benny Gantz, amesema usiku wa jana kwamba kumekuwepo majaribio mapya yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, ambayo amesema yanaweza kusitisha vita huko Gaza. Lakini Gantz amesisitiza kuwa hilo litawezekana ikiwa tu Hamas itakubali kuwaachilia mateka wa Israel waliosalia kwenye Ukanda wa Gaza.
Mnamo majuzi, Israel ilitishia kuwa itaanzisha mashambulizi ya ardhini katika mji wa kusini mwa Gaza na wenye watu wengi wa Rafah katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameielezea hali mbaya inayoendelea huko Gaza:
" Washirika wetu wa kibinadamu wanaoshughulikia masuala ya maji, usafi wa mazingira na afya huko Gaza walionya jana kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na janga la kiafya linalotokea katika Ukanda wa Gaza. Watu wengi hawajapata maji safi, na moja tu ya mabomba matatu kutoka Israel ndio bado yanafanya kazi, tena ikiwa chini ya nusu ya uwezo wake wa kawaida. Takriban asilimia 83 ya visima havitumiki tena huko Gaza, huku mifumo ya maji taka ikiwa yote haifanyi kazi."
Miito ya usitishwaji mapigano huko Gaza yatolewa
Wakati wa mazungumzo katika mkutano wa G20 huko Brazil, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua jukumu kubwa la kushinikiza usitishaji haraka wa vita vya Gaza na pia kuwepo kwa suluhu ya mataifa mawili.
Soma pia: Vurugu bungeni Uingereza kwa maazimio ya Gaza
Wito kama huo umetolewa pia na Mratibu wa Shirika la Misaada ya Dharura la Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ambaye amewataka mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 20 zilizoendelea na kustawi kiviwanda kuchukua hatua za kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.
Jana, Bunge la Israel liliunga mkono kwa wingi pendekezo la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu la kupinga uamuzi wa upande mmoja wa kutambuliwa kwa taifa la Palestina. Netanyahu amekuwa mara kadha akisisitiza kuwa Israel itaendeleza mashambulizi yake huko Gaza hadi watakapopata kile anachokiita "ushindi kamili".
(Vyanzo:afp,ap,rtr,dpa)