Felicien Kabuga afikishwa mahakama ya The Hague
11 Novemba 2020Kabuga mwenye umri wa miaka 84, amekuwa mafichoni kwa zaidi ya miongo miwili na ni mtu anaesakwa zaidi ulimwenguni. Anatuhumiwa kwa kuchochea mauaji ya Watutsi 800,000 pamoja na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Miaka hiyo Kabuga alikuwa akizingatiwa kama mtu tajiri zaidi Rwanda. Na anadaiwa alitumia utajiri wake kuanzisha vyombo vya habari vilivyokuwa vikisambaza taarifa za chuki zilizokuwa zikiwachochea Wahutu kuwauwa wenzao wa kabila la Tutsi kwa kutumia maneno ya propaganda na kuwaita mende ili kuwatoa utu wao, iwe rahisi kuwaua.
Soma zaidi: Wanyarwanda wataka Kabuga ashtakiwe nyumbani
Alikamatwa karibu na mji wa Paris mnamo Mei 16 na anakabiliwa na mashtaka ya mwaka 1997 ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) iliyofungwa sasa. Kabuga alihamishwa kutoka Ufaransa kwenda mjini The Hague mnamo mwezi Oktoba.
Leo mchana atakutana na jaji kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa rasmi, katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa iIiyoanzishwa kwa ajili ya kusikiliza kesi za uhalifu, IRMCT, ambayo imechukua kesi zilizobakia kutoka mahakama ya ICTR.
Jaji huyo amesema kwamba Kabuga anaweza kuhudhuria kibinafsi au kupitia njia ya video. Ripoti ya awali ya matibabu imependekeza mkutano huwo ufanyike kwa njia ya video kwa sababu ya janga la virusi vya corona.
Kabuga alisaidiwa kujificha na washirika wake wa zamani wa Rwanda
Kulingana na Umoja wa Mataifa watu 800,000 waliuawa katika ghasia hizo za siku 100 zilizoanza Aprili 1994.
Kabuga anadaiwa alisaidia kuunda kikundi cha wanamgambo cha Wahutu kilichoitwa Interahamwe, pamoja na kuanzisha kituo cha Redio na Televisheni kwa jina la Libre des Mille Collines ambavyo matangazo yake yalikuwa yakichochea watu kuuwana.
Soma zaidi: Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda akamatwa
Anatuhumiwa pia kusaidia kununua mapanga mnamo mwaka 1993 ambayo yaligawanywa katika vikundi vilivyokuwa vikifanya mauaji.
Kabuga hata hivyo amekanusha mashtaka yote hayo dhidi yake.
Kwa miaka mingi Kabuga amekuwa mafichoni akitumia paspoti za uwongo huku wachunguzi wakisema kwamba alikuwa akisaidiwa na mtandao wa washirika wake wa zamani wa Rwanda kukwepa haki.
Kufuatia kukamatwa kwake, mawakili wake walitaka kesi yake isikilizwe nchini Ufaransa, lakini mahakama ya juu nchini humo imeamrisha kesi hiyo ihamishiwe kwenye mahakama ya Umoja wa Mataifa.
Chanzo: afp