Kagame amtuhumu Tshisekedi kutumia M23 kuahirisha uchaguzi
1 Desemba 2022Mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Congo na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa Congo yamechochea zaidi mzozo na Rwanda, ambayo Congo inaishtumu kuunga mkono uasi wa kundi hilo, madai ambayo Rwanda inayakanusha.
Mazungumzo kati ya Congo na Rwanda nchini Angola wiki iliyopita yalizaa mapatano ya kusitisha mapigano, na siku kadhaa baadae, mapatano hayo yanaonekena kuendelea kuheshimiwa.
Soma pia:Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023.
Katika hotuba ya kiserikali, Kagame alisema "dunia nzima" inaelekeza lawama za mzozo huo kwa Rwanda lakini ni rais wa DRC Felix Tshisekedi anaetafuta kujinufaisha kutokana na machafuko hayo mnamo wakati uchaguzi ukikaribia.
"Tatizo hili linaweza kutatuliwa ikiwa nchi moja inayoelekea kenye uchaguzi mwakani, haijaribu kuunda mazingira ya dharura ili uchaguzi usifanyike", Kagame alisema katika hafla ya kuwaapisha mawaziri wapya.
Soma pia: Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano
"Ikiwa anajaribu kutafuta njia nyingine ya kuahirisha uchaguzi ujao, basi ingekuwa vyema akatumia visingizio vingine,na siyo sisi."
CENI: Hali ya usalama kutoa changamoto kwa uchaguzi
Tshisekedi aliingia madarakani Januari 2019 na DRC itafanya uchaguzi wa rais Desemba 2023.
Soma pia: Kenyatta na Kagame waitaka M23 kusitisha mapigano na kujiondoa mashariki mwa Kongo
Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo CENI, ilisema mwezi uliopita kwamba ukosefu wa usalama unaoendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi yatasabisha changamoto kwa kura huru, ya kidemokrasia na ya wazi.
DRC na Rwanda zimeshtumiana kwa kuunga mkono makundi ya waasi na kurejea tena kwa M23 kumezidisha upya mzozo wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo.
Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yalioanza kutekelezwa Novemba 25, wapiganaji wa M23 walipaswa kujiondoa kutoka maeneo walioyakalia mashariki mwa Congo, na kushindwa kufanya hivyo kikosi cha Afrika Mashariki kitaingilia kati kuwalaazimisha.
Duru nyingine ya mazungumzo na makundi ya waasi iliendelea nchini Kenya siku ya Jumatano, bila kuwepo wawakilishi wa M23.
Mpatanishi wa mazungumzo hayo, rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alisema makundi ya waasi ya kigeni yanayoendesha shaghuli zao nchini Congo yanapaswa kuondoka au yakabiliwe na majeshi ya DRC na Afrika Mashariki.
Tayari wamepewa ilani: DRC haitakuwa mahala pa mapigano ya mataifa mengine, alisema Kenyatta.
Chanzo: AFP