Kamari ya Merkel kwa Uturuki
10 Machi 2016Baada ya kuwafungulia milango wakimbizi wa Syria wanaoingia Ulaya mwezi Septemba na kuwashtua viongozi wengi wa Ulaya ambao hawakushauriwa, Merkel sasa amecheza kamari ya dakika za mwisho kwa kufikia makubaliano na Uturuki, yenye lengo la kusitisha mmiminiko wa wakimbizi.
Iwapo mkakati huo uliobuniwa usiku wa manane wiki moja kabla ya uchaguzi muhimu wa majimbo nchini Ujerumani, ambamo chama chake kinakabiliwa na kushindwa - utageuka kuwa wa mafanikio au bomu katika mgogoro wa wakimbizi - ni suala linalosubiriwa.
Hisia za Wajerumani kuhusu makubaliano na Uturuki ni mchanganyiko. Gazeti linaloongoza kwa mauzo nchini humo la Bild, liliyakaribisha kwa kicha cha habari kisemacho: "mpira sasa uko mikoni mwa Uturuki," lakini baadhi ya wabunge wa chama chake cha kihafidhina, wanapinga kuiondolewa Uturuki sharti la viza kama moja ya vipengele muhimu vya makubaliano hayo.
Davutoglu ndiye mshindi
Maafisa wa Ujerumani wanasema alikuwa waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu aliewashangaza wengi kwa kuwasili kwenye mkutano na Merkel na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte mjini Brussles siku ya Jumapili usiku, akiwa na mpango wa dhahiri wa kuwapokea tena wahamiaji wote wanaovuka na kuingia Ulaya, kwa kupatiwa upendeleo wa kiuchumi na kisiasa.
Wanadiplomasia na maafisa wa Ulaya mjini Brussels walishangazwa na pendekezo hilo walilopatiwa wakati wa mkutano wa kilele siku ya Jumatatu, huku baadhi wakikasirika kwa kuachwa gizani wakati wa maandalizi yake.
Mmoja wao alipoulizwa ni namna gani wazo la kuwarejesha Uturuki wahamiaji wakiwemo wakimbizi wa Syira litakapofanya kazi, alisema "Muulize bibi Merkel." Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk - ambaye aliongoza mkutano wa Jumatatu, alitumia siku mbili mjini Ankara na Istanbul wili illiyopita akishughulikia makubaliano mengine, na hakuwa anajua zaidi kilichokuwa njiani.
Si Tusk wala rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker aliealikwa kwenye kikao cha maandalizi Jumapili usiku. Hata Ufaransa, mshirika wa karibu zaidi wa Ujerumani barani Ulaya haikushirkishwa.
Mark Rutte badalya ya Francoise Hollande
Wakati Merkel alimshirikisha rais Francoise Hollande katika diplomasia yake na Urusi kuhusiana na mgogoro wa Ukraine, mara hii alimgeukia Mark Rutte wa Uholanzi kama mmoja wa viongozi wachache walio tayari kuchukuwa wakimbizi wa Syria moja kwa moja kutoka Uturuki.
Wanadiplomsia walisema wakati baadhi ya viongozi walipomuuliza Tusk kwa nini hakuwaarifu kuhusu mpango wa Uturuki baada ya ziara yake, alikiri kuwa hakufahamu kuhusu pendekezo muhimu la kuwarudisha wahamiaji nchini Uturuki hadi Jumatatu asubuhi.
Waziri mkuu huyo wa zamani wa Poland alijikuta akiburutwa katika mvutano kati ya Merkel na Kansela wa Austria Wermer Feymann, ambaye alimkarisha Merkel kwa kuitisha mkutano wa mataifa ya Ulaya ya Kati na Balkan mwezi uliyopita, bila Ujerumani au Ugiriki, kuratibu ufungaji wa mipaka yao kwa wahamiaji.
Ingawa Merkel amekanusha kuwa na malengo ya ndani katika makubaliano na Uturuki, lakini yanatoa ishara muhimu kuelekea uchaguzi katika majimbo ya Baden-Würtenberg, Rhineland-Pfalz na Saxony-Anhalt ambao huenda ukaamuwa mustakabali wake wa kisiasa.
Kiongozi wa aina yake
Kushindwa vibaya kwa chama chake cha CDU kunaweza kumdhofisha na kuibuwa maswali kuhusiana na uwezo wake wa kukiongoza chama kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao, ingawa umaarufu wake bado uko juu na hakuna kiongozi mbadala kwake mpaka wakati huu.
Pamoja na kutoridhishwa kwao, viongozi wengi wa Umoja wa Ulaya wanasita kumpinga Merkel, kiongozi wa taifa mwanachama wa umoja huo lenye nguvu zaidi katika wakati ambapo ana uhitaji mkubwa zaidi wa kuungwa mkono kisiasa.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo