KAMPALA: Rais Museveni azuru Juba
21 Oktoba 2006Rais wa Uganda, Yoweri Museveni leo amekutana na maofisa wa kusini mwa Sudan mjini Juba. Ziara yake ya siku moja mjini Juba imelenga kuyapa nguvu mazungumzo ya amani yenye nia ya kumaliza miongo miwili ya upinzani mkali nchini mwake.
Wakati huo huo, jeshi la Uganda limewekwa katika hali ya tahadhari kufuatia hatua ya serikali kutangaza kuufunga mpaka wake na Sudan kwa muda.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya watu wasiojulikana kuwashambulia na kuwaua watu 38 katika barabara zinazoelekea mjini Juba, kusini mwa Sudan. Msemaji wa jeshi la Uganda, meja Felix Kulaije, amesema mpaka huo utafunguliwa mara tu usalama utakapoimarishwa.
Aidha meja Kulaije amesema hakuna magari yanayoruhusiwa kwenda Sudan kwa sababu ya hali mbaya ya usalama. Amedai kwamba kundi la waasi la Lord´s Resistance Army, limehusika na mauaji hayo ambayo amesema yalifanywa mnamo Jumatano iliyopita.
Msemaji wa kundi la LRA, Godfrey Ayo, amekanusha madai hayo akisema hawakuhusika. Mamia ya abiria waliotaka kwenda kusini wa Sudan wamekwama mpakani.