1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani hatopeleka makombora ya masafa marefu Ukraine

Angela Mdungu
15 Septemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kuwa nchi yake haitapeleka makombora ya masafa marefu aina ya Taurus nchini Ukraine, licha ya uamuzi uliofanywa na nchi nyingine washirika.

https://p.dw.com/p/4ke1g
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza nchi yake haitaipatia Ukraine makombora ya Taurus
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Ameendelea kuushikilia msimamo huo alipokuwa akifanya mazungumzo na wananchi katika mji wa Prenzlau jimboni Brandenburg. Scholz ameeleza kuwa kuyapeleka Ukraine makombora ya Taurus yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 500 kutazidi kuhatarisha hali katika mzozo huo.

Soma zaidi: Ukraine yaihimiza Ujerumani kuipatia makombora ya Taurus

Mataifa washirika  yaliyo chini ya Jumuiya ya kujihami ya NATO, ambayo ni Marekani, Uingereza na Ufaransa, yamekubali kuipatia Ukraine makombora yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 300 licha ya kuendelea kwa mjadala ikiwa makombora hayo yaidhinishwe kutumiwa dhidi ya maeneo ya Urusi  ama la.

Soma zaidi: Bunge la Ujerumani lakataa kuitumia Ukraine makombora ya masafa marefu

Rais Vladmir Putin wa Urusi ameshasema kuwa atayatizama matumizi ya makombora ya masafa marefu ndani ya ardhi yake kuwa ni uhusika wa moja kwa moja wa Jumuiya ya kujihami ya NATO katika vita hivyo.