Austria: Kansela Kurz kujiuzulu kwa tuhuma za rushwa
9 Oktoba 2021Kurz amekuwa akikabiliwa na tuhuma kwamba chama anachokiongoza kilitumia fedha za serikali kujiunufaisha na fadhila ya vyombo vya habari.
Soma zaidi: Kurz ashinda uchaguzi wa Austria
Baada ya kukaidi miito ya kumtaka ajiuzulu, hatimaye Jumamosi usiku alisalimu amri, na kutangaza kuwa anajiengua madarakani kutokana na shutuma hizo kwamba ofisi yake ilivuja fedha za umma.
Kurz amesema ataingia bungeni kama kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Austrian People's Party (ÖVP), na kwamba waziri wa mambo ya nje, Alexander Schallenberg atajaza nafasi yake kama kansela.
''Nchi yangu ni muhimu kwangu kuliko mimi,'' amesema Kurz katika hotuba yake kwa njia ya televisheni.
''Tunachokihitaji sasa ni utulivu,'' amewaambia waandishi wa habari mjini Vienna, na kuongeza kuwa anajiweka kando ili kuepusha mkwamo na kuzuia ghasia.
Shutuma zinazomwandama Kurz
Mapema wiki hii, mwendeshamashitaka mkuu wa Austria alisema Kansela Kurz na watu wengine tisa walikuwa wakichunguzwa kwa rushwa baada ya wapelelezi kufanya msako katika ofisi za chama tawala.
Soma zaidi: Austria wapigakura wahafidhina wakionekana kuongoza
Ingawa chama hicho, ÖVP kilisimama naye wakati wa shutuma dhidi yake, chama cha kijani ambacho ni mshirika katika serikali ya muungano, Ijumaa kilimtaka Kansela Kurz kufungasha vyake na kuondoka.
Kiongozi wa chama cha Kijani ambaye pia ni Naibu Kansela Werner Kogler alitoa hoja kwamba Kurz 'hafai tena' kuiongoza ofisi yake, na kukitaka chama cha ÖVP kumtafuta mtu mwingine 'muadilifu' ili kuchukua nafasi yake.
Kurz na washirika wake wanatuhumiwa kutumia fedha za serikali kutoka wizara ya fedha, 'kugharimia ulaghai wa kupindisha utafiti wa maoni, kwa manufaa ya kisiasa' ya chama chake kati ya mwaka 2016 na 2018.
Mwaka 2017 Sebastian Kurz alichukuwa oungozi wa chama cha ÖVP cha mrengo wa kulia, na baadaye kuwa kansela akiongoza serikali ya muungano na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Freedon Party (FPÖ).
Soma zaidi: Naibu Kansela wa Austria Heinz-Christian Strache ajiuzulu
Sasa yeye, watu wengine tisa na mashirika matatu, wanachunguzwa wakishukiwa kufanya uhalifu, wamesema waendeshamashtaka.
Alipokuwa akitangaza azma ya kujiuzulu Jumamosi usiku, Kurz kwa mara nyingine alisema shutuma dhidi yake ni uongo mtupu, na kwamba anaamini kwa dhati kwamba ataweza kusafisha jina lake.
Ngwe ya pili kama kansela
Kurz alijiuzulu ukansela mwara ya kwanza Mei 2019, hatua iliyoisambaratisha serikali ya muungano wa chama chake na kile cha FPÖ, kuhusiana na kashfa nyingine iliyojulikana kama Ibiza-gate ambayo pia ilikuwa a ufisadi.
Mkanda wa vidio uliibuka ukimuonyesha mkuu wa chama cha FPÖ Heinz-Christian Strache - akiwa naibu kansela wakati huo - akionekana kutoa zabuni ya umma kwa kampuni ambayo ingemlipa kwa kufadhili kampeni yake.
Soma zaidi: Austria kufanya uchaguzi wa mapema Septemba:
Tangu kisa hicho, uchunguzi umekuwa ukifanyika juu ya ashutuma za rushwa, baadhi zikiwa dhidi ya wanasiasa wakuu wa ÖVP, akiwemo waziri wa fedha Blümel.
Sebastian Kurz alianza ngwe ya pili kama mkuu wa serikali ya Austria Januari 2020, akiongoza muungano wa chama chake na chama cha Kijani kama mshirika mdogo serikalini.
rtre, afpe, dpae