1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz azuru Ukraine

2 Desemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amefanya ziara ya kushtukiza nchini Ukraine leo Jumatatu akilenga kuthibitisha kwa mara nyingine uungwaji mkono kwa taifa hilo, linalopigana vita na Urusi.

https://p.dw.com/p/4nddW
Poland | 2024
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwa nchini Poland, tayari kuanza safari ya treni kuelekea mjini Kyiv katika ziara ya kushtukiza ya kuonyesha mshikamano na UkrainePicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Scholz anafanya ziara hii wakati wanajeshi wa Ukraine walioko mstari wa mbele wakionekana kuelemewa na katikati ya wasiwasi kuhusu mustakabali wa msaada wa Marekani nchini Ukraine. 

"Nimekwenda Ukraine kwa kutumia treni na tutaendelea kusimama pamoja na Ukraine," aliandika Kansela Sholz kwenye ukurasa wa X. Aidha aliahidi msaada zaidi wa kijeshi wa yuro milioni 650 ambao utapelekwa Ukraine kabla ya mwisho wa mwaka. Alitoa ahadi hii alipokutana na Rais Volodymyr Zelensky. 

Sholz anazuru Ukraine wakati taarifa zikisema, wanajeshi wa Ukraine walioko msitari wa mbele wameelemewa na vita. Na kwa upande mwingine, Urusi inashambulia miundombinu ya nishati na kuongeza mashaka kwa watu wa nchi hiyo inayoingia kwenye majira ya baridi kali.

Lakini pia wasiwasi wa wasiwasi wa Marekani kuondoa msaada wa kijeshi kwa taifa hilo mara baada ya Rais mteule Donald Trump kuingia madarakani mwezi Januari mwakani, nacho ni kitisho kingine kinachoweza kuongeza ugumu zaidi kwa upande wa Ukraine inayopigana na Urusi kwa zaidi ya siku 1,000 sasa.

Kansela Scholz aidha ametoa wito wa juhudi za kijeshi lakini pia za kidiplomasia katika harakati za kuvimaliza vita hivyo, katika namna ambayo italinda uhuru wa Ukraine. Chini ya uongozi wake, Ujerumani inayotarajiwa kufanya uchaguzi mpya mwezi Februari, imekuwa kinara wa Ulaya katika kuisaidia Ukraine, ikiifutia Marekani, ingawa ilikataa katakata kupeleka makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kushambulia ndani ya Urusi.

Scholz aihimiza Urusi kukubaliana na Ukraine ili kufikia amani 

Rais Vladimir Putin na Olaf Scholz
Picha ya pamoja na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani. Hivi karibuni viongozi hawa walizungumza na siku kuhusiana na mustakabali wa mzozo kati ya Urusi na UkrainePicha: Kay Nietfeld/Sputnik/AP/dpa/picture alliance

Na katikati ya mwezi Novemba, Scholz alizungumza kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa Urusi na kuwa kiongozi wa kwanza wa Ulaya kufanya mazungumzo kama hayo yaliyopingwa vikali na Zelensky. Kwenye mazungumzo, Scholz alitolea wito Urusi kuonyesha nia ya kukubaliana na Ukraine kwa lengo la kufikia amani ya haki na ya kudumu.

Soma pia:Scholz afanya mazungumzo ya kwanza rasmi kwa njia ya simu tangu kuzungumza na Putin

Zelensky alisema jana Jumapili kwamba Jumuiya ya Kujihami, NATO inatakiwa kuwahakikishia usalama na kuwapatia silaha zaidi za kujitetea kabla ya mazungumzo yoyote na Urusi.

Ametoa matamshi hayo baada ya mkutano na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas pamoja na Mkuu wa Baraza la umoja huo, Antonio Costa, ambao walizuru Kyiv kama ishara ya kuendeleza uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya mara baada ya viongozi hao kushika nyadhifa hizo mpya.

Soma pia:Zelensky aiomba NATO kuimarisha ulinzi kwenye baadhi ya maeneo inayoyadhibiti

Huko Kyiv, kumeshuhudiwa msururu wa mashambulizi ya droni yaliyofanywa na Urusi kwa usiku mzima wa kuamkia leo na kumuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine watatu katika mji wa Ternopil kaskazini mwa Ukraine, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za Kyiv. Moto uliozuka kwenye jengo lililoshambuliwa uliharibu makazi 20 na taasisi ya elimu iliyoko karibu na jengo hilo.

Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi iliwashambulia kwa droni 110, ikiwa ni pamoja na zile zinazotengenezwa Urusi. Lakini jeshi hilo lilifanikiwa kuzindugua droni 52 na nyingine 50 zilipotea, ingawa jeshi hilo limesema huenda ziliangushwa na mifumo ya kieleketroniki ya kujilinda.