Katumbi asitisha kampeni zake baada ya vurugu Kongo
13 Desemba 2023Hii ni baada ya kuibuka kwa mapigano makali katika moja ya mikutano yake wakati wa kampeni za uchaguzi.
Soma pia: Uchochezi wa vita, ukabila vyatawala kwenye kampeni Kongo
Watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya risasi za moto kufyatuliwa wakati Katumbi akiwahutubia wafuasi katika mji wa pwani wa Moanda, hatua inayoashiria kuongezeka kwa mvutano kabla ya uchaguzi wa Desemba 20.
Hata hivyo, kuna maelezo tofauti ya tukio hilo, huku serikali ya mkoa ikisema katika taarifa yake kwamba walinzi wa Katumbi walifyatua risasi hewani kama onyo baada ya umati wa watu kuongezeka na kuibua fujo, na kuchochea mvutano na malumbano. Polisi walitumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya utulivu.
Lakini kwenye ukurasa wake wa X, Katumbi amesema polisi walifyatua risasi za moto dhidi ya raia na kwamba tukio hilo lilipangwa kuchochea vurugu.
Soma pia: Marekani : Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa saa 72 yakubaliwa Mashariki mwa Kongo
Taarifa ya serikali imesema pia watu kadhaa walijeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi ambaye aliumia vibaya, na uchunguzi unaendelea.
Katumbi amesema ili kuepusha uchochezi zaidi, ameamua kusimamisha kwa muda mkutano wake na wananchi katika miji ya Kananga na Tshikapa katika jimbo la Kasai-Kati, ambayo ni ngome ya Rais Felix Tshisekedi.
Changamoto zilizopo
Takriban watu milioni 44 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi utakaoamua iwapo rais Tshisekediatasalia madarakani baada ya muhula wa kwanza uliokumbwa na matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa usalama.
Katumbi ni mmoja wa wagombea katika kinyang'anyiro cha urais ambacho kinawajumuisha pia viongozi wakuu wa upinzani kama Martin Fayulu na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel daktari wa magonjwa ya wanawake Denis Mukwege.
Soma pia: M23 wakamata mji mashariki mwa Kongo
Kumekuwa na changamoto kadhaa katika maandalizi ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na madai ya kasoro katika uandikishaji wa wapiga kura na ugumu wa kusambaza vifaa vya kupigia kura.
Wiki iliyopita, tume ya uchaguzi iliiambia ofisi ya rais kwamba ilihitaji haraka ndege nne kubwa na helikopta 10 ili kusafirisha vifaa vya uchaguzi katika maeneo yote.
Soma pia: Changamoto zaongezeka wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu Congo
Ingawa baadhi ya waangalizi wanatilia shaka uchaguzi huo iwapo unaweza kufanyika ipasavyo, tume yauchaguzi inashikilia kuwa ratiba itaheshimiwa ili kufanikisha upigaji kura kwa takriban wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha.