Kenya, EU wakaribia kukamilisha makubaliano ya biashara
18 Desemba 2023"Makubaliano ya leo yanaanzisha ukurasa mpya ambapo bidhaa za Kenya zitaruhusiwa kuingia soko la Ulaya mara moja kutozwa ushuru na bila kiwango cha ukomo," Waziri wa Biashara wa Kenya Rebecca Miano alisema kabla ya kutia saini mkataba wa kibiashara katika hafla iliyofanyika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Jumatatu.
"Baada ya muda, bidhaa za Ulaya pia zitapata fursa ya upendeleo katika soko la Kenya," aliongeza.
Baraza la Umoja wa Ulaya liliidhinisha makubaliano hayo ya kibiashara wiki iliyopita, lakini bado yanahitaji kuidhinishwa na bunge la Kenya na Bunge la Ulaya kabla ya kuanza kutumika.
"Kiini cha mpango huu ni kuweka pesa halisi katika mifuko ya watu wa kawaida," Rais wa Kenya William Ruto alisema katika hafla ya kutia saini.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, ambaye pia alihudhuria tukio hilo, aliuita ushirikiano huo "hali ya ushindi wa pande mbili."
Mkataba huo unakuja wakati Brussels ikitafuta uhusiano thabiti wa kiuchumi na Afrika ili kukabiliana na ushawishi wa China, huku ikihimiza ahadi za maendeleo kati ya EU na Kenya katika maeneo ikiwa ni pamoja na ulinzi wa mazingira na haki za wafanyikazi.
Mauzo ya nje bila ushuru na bila ukomo
Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya EU-Kenya (EPA), ambayo yalikamilishwa Juni 2023, yanahakikisha uingizwaji bila ushuru na bila ukomo wa bidhaa zinazotoka nchini Kenya katika jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 27, ukiacha silaha.
Umoja wa Ulaya ndiyo soko muhimu zaidi la mauzo ya nje na mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibishara.
Mwaka 2022, Kenya ilisafirisha bidhaa za thamani ya euro bilioni 1.2, hasa za kilimo katika Umoja wa Ulaya, ikiwemo chai, kahawa, maua, njegere na maharage. Zaidi ya theluthi mbili, au asilimia 70 ya uzalishaji wa maua ya Kenya yanauzwa katika soko la Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wa Kenya, yenye uchumi mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki, itafungua hatua kwa hatua soko lake kwa bidhaa za Ulaya, huku makubaliano yakishuhudia ushuru ukipunguzwa katika kipindi cha miaka 25. Kwa sasa, Kenya inaagiza hasa mashine na bidhaa za madini na kemikali kutoka EU.
Kenya itaweza kulinda baadhi ya zinazoitwa "bidhaa nyeti," ama kwa kuzitenga na na kupunguzwa kwa ushuru au kuanzisha ulinzi endapo kutakuwa na ongezeko la ghafla la bidhaa kutoka EU.
Soma pia: Afrika Mashariki yalia na EU makubaliano ya EPA
Makubaliano hayo yanakuja huku biashara kati ya EU na Kenya ikiongezeka kwa asilimia 27 kutoka 2018 hadi 2022.
EPA ndiyo mkataba wa karibuni zaidi wa kibiashara kati ya EU na taifa la Afrika tangu EU ilipotia saini makubaliano sawa na Ghana mwaka 2016.
Nini maana ya EPA kwa Kenya?
"Ni wakati mzuri wa kuwa na makubaliano ambayo yanaweza kusaidia kubadilisha bidhaa zinazouzwa Kenya na washirika wa kibiashara katika Umoja wa Ulaya," alisema Sherillyn Raga, mtafiti mwenza katika Taasisi ya Maendeleo ya Ng'ambo.
Uholanzi, Ujerumani na Ufaransa kwa sasa ndizo zinazoongoza kwa uagizaji wa bidhaa za Kenya katika Umoja wa Ulaya.
Ulimwengu umekumbwa na misukosuko mingi ya kiuchumi kuanzia janga la COVID-19 na athari za vita vya Urusi nchini Ukraine hadi mabadiliko ya tabianchi. "Muundo wako wa biashara unapojikita kwenye idadi ndogo ya washirika au idadi ndogo ya bidhaa, basi uko katika hatari kubwa ya mabadiliko ya bei za kimataifa," alisema Raga, mtaalamu wa uchumi mkuu na mchambuzi wa biashara, akiongeza kuwa kwa sababu ya hii, " mseto wa kibiashara ni njia mojawapo ya kuongeza ustahimilivu wa Kenya dhidi ya majanga."
Kwa mauzo ya Kenya ndani ya EU, hata hivyo, mpango huo hautabadili mengi katika muda mfupi. Kenya tayari inafurahia biashara isiyo na ushuru na upendeleo na EU chini ya mpango maalum wa muda, ambao uliwekwa mnamo 2014 baada ya makubaliano ambayo EU ilijadiliana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukwama.
Soma pia: Ukanda huru wa biashara Afrika wazinduliwa
Kile ambacho makubaliano ya hivi sasa yanafanya, kwanza kabisa, ni kufunagua rasmi soko la Umoja wa Ulaya kwa bidhaa za Kenya, na hivyo "kupunguza mashaka," alisema mwanauchumi Frederik Stender, ambaye anashughulikia sera za biashara na masuala ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda katika Taasisi ya Maendeleo na Unedelevu ya Ujerumani.
Hii, inaweza kuvutia uwekezaji na ufadhili wa Umoja wa Ulaya katika muda wa kati hadi mrefu.
Jambo la kuzingiatia ni kwamba makubaliano hayo ya biashara hayahusu tu biashara. Pia yana "mtazamo wa maendeleo" kwa Kenya, Stender alisema. Kenya imekubali kutekeleza ahadi za lazima zinazohusiana na ulinzi wa mazingira, hatua za tabianchi, kupiga vita ukosefu wa usawa wa kijinsia na kuimarisha haki za wafanyikazi.
Makubaliano hayo pia yanahusisha msaada unaohusiana na maendeleo ya biashara ili kukabiliana na baadhi mambo yanayozuwia mauzo ya nje ya Kenya, kama vile ukosefu wa uwezo wa uzalishaji, miundombinu, rasilimali watu na uwezo wa kuzingatia viwango vya EU, Stender alisema.
Soma pia: Mkutano wa umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika kuhusu EPA waingia mtafaruku.
Vipengele kama hivyo, inatumainiwa vitasaidia wauzaji bidhaa wa Kenya kuvuka baadhi ya vikwazo wanavyokumbana navyo katika kufanya biashara na EU, na hatimaye vinaweza kuisaidia Kenya kuunganishwa vyema katika mifumo ya thamani ya EU.
Utafiti wa 2021 kuhusu fursa za mauzo ya nje ya Kenya ulioandikwa na Raga ulibaini kuwa vikwazo vingi vya kuingia katika soko la Umoja wa Ulaya vinazingatia mahitaji ya Umoja wa Ulaya ya kuweka lebo, hatua zinazohitajika kudhibiti magonjwa ya mimea na kulinda afya ya mimea, inayojulikana kama udhibiti wa phytosanitary, na sheria za chimbuko.
Kwanini Kenya ilifikia makubaliano na EU bila Jumuiya ya Afrika Mashariki?
Mwaka 2014, mataifa wanachama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya, Rwanda, Burundi, Tanzania na Uganda yalijadili Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Umoja wa Ulaya. Lakini ni Kenya pekee iliyoendelea kuidhinisha mpango huo. Bila saini za wanachama wengine wa EAC, ambayo sasa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini, makubaliano ya biashara huria ya EU-EAC hayangeweza kutekelezwa.
Wanachama wengine wa EAC walihisi shinikizo kidogo la kuridhia makubaliano ya pamoja kwa sababu tayari zinalifikia soko la EU bila ukomo kupitia hadhi yao ya kuorodheshwa kwa mataifa yenye maendeleo duni. Lakini kama nchi yenye uchumi wa pato la kati-chini, Kenya haifurahii kipengele hicho.
Mapema 2021, wakuu wa nchi za EAC walikubali kuyaruhusu mataifa wanachama binafsi wanaotaka kutekeleza makubaliano ya biashara ya Umoja wa Ulaya kujadiliana moja kwa moja na Umoja wa Ulaya. Wanachama wa EAC wote wanakaribishwa mmoja mmoja kujiunga na mkataba mpya wa kibiashara, Rais Ruto alisema katika hafla mwezi Desemba.
"Mkataba huu tunaotia saini leo unaacha mlango wazi, na nasema, wazi kabisaa, kwa washirika wetu wa EAC kujiunga," Ruto alisema.
Katika hotuba yake, Rais wa Halmashauri Kuu ya EU, Ursula von der Leyen, pia alizihimiza nchi nyingine za Afrika Mashariki kujiunga na makubaliano hayo.
Vipi kuhusu mikataba mingine ya biashara ya Kenya?
Maendeleo ya polepole ya ushirikiano wa kikanda barani Afrika pengine ndiyo sababu iliyoisukuma Kenya kujadili mkataba wa biashara wa EU na inatazamia kufunga mengine.
Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika lilianza kufanya kazi mwaka wa 2019, na awamu yake ya uendeshaji ilianza mwaka wa 2021, lakini hadi sasa ni nchi kadhaa tu, ikiwa ni pamoja na Kenya, ambazo zimeanza kwa muda kufanya biashara ya bidhaa zilizochaguliwa kwa majaribio.
Kutokana na hali hii, Kenya inaonekana kutafuta ushirikiano wa karibu na washirika wengine nje ya Afrika. Kenya ilitia saini mkataba sawa wa kibiashara na Uingereza mnamo Desemba 2020, wakati Uingereza ilipojiondoa katika Umoja wa Ulaya.
Taifa hilo la Afrika Mashariki pia linajadiliana kuhusu mkataba wa kibiashara na Marekani, ambao unaweza kutiwa saini mwaka ujao. Kenya inauza bidhaa zake katika soko la marekani bila ushuru hadi mwaka 2025 chini ya mpango wa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika, AGOA. Lakini kama ilivyo kwa Umoja wa Ulaya, kuwa na makubaliano rasmi na ya kudumu kunaweza kuvutia uwekezaji zaidi.
Kenya pia iko katika mazungumzo na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambapo mataifa hayo mawili yalisaini mnamo Julai 2022 makubaliano ya nia ya kuanza mazungumzo kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi.
Soma pia:Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika wamalizika mjini Lisbon
Iwapo makubaliano yatakamilika, yatakuwa ya kwanza ya kibiashara kati ya nchi hiyo ya Kiarabu na yenye utajiri wa mafuta na taifa la Kiafrika. Kama mojawapo ya washirika muhimu zaidi wa mauzo ya nje wa Kenya, UAE inachukuliwa kuwa muhimu kwa biashara na uwekezaji na Mashariki ya Kati. Bidhaa kuu za mauzo ya Kenya kwa UAE ni petroli iliyosafishwa, chai, nyama ya kondoo na mbuzi.
Biashara kati ya nchi hizo mbili kwa sasa ina ukosefu mkubwa wa usawa unaoipendelea UAE, ambayo iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.8 kwa Kenya huku ikiagiza bidhaa za dola milioni 328 tu kutoka Kenya.
Kenya imesema ina nia ya kukuza biashara yake isiyo ya mafuta na UAE, kama vile nazi na viazi vya Kenya, miongoni mwa bidhaa nyingine za kilimo.
"Kenya inafanya kila iwezalo kupata baadhi ya mikataba ili iweze kupanua mauzo yake ya nje na kubadilisha washirika wake wa mauzo ya nje na biashara," alisema Raga, akiongeza kuwa Kenya inaweza kuweka mfano kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki juu ya namna mikataba hiyo ya kibiashara inavyoweza kuonekana.