1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Wawindaji haramu wa ndovu watiwa mbaroni

Miraji Othman1 Desemba 2009

Interpol: Msako wa kuwalinda ndovu wa Afrika

https://p.dw.com/p/Kn9x
Bandari ya Mombasa,Kenya, moja ya malengo ya polisi wa kimataifa kwanaotafuta pembe za ndovu zinazosafirishwa ng'ambo kwa njia ya magendoPicha: picture-alliance/ dpa

Hatua ya mwishoni ya kuowanisha operesheni ya polisi wa kimataifa katika nchi sita za Kiafrika imepelekea kukamatwa kilo 568 za meno ya ndovu zilizopatikana kwa njia ya haramu na kukamatwa watu 65, wakiwemo raia watatu wa Kichina. Hayo yameelezwa na Idara ya Wanyama wa Porini ya Kenya. Ni chini ya kilo 1,800 zilizotwaaliwa kwa ujumla katika operesheni hiyo, zikiwemo shehena mbili za meno ya ndovu zilizokuwa zinataka kupelekwa Bangkok, meno hayo yakiwa yale yaliochongwa na yasiochongwa kutokea Kenya na Ethiopia mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Hatua hii ya karibuni sana ilio kubwa kabisa kufanywa dhidi ya wawindaji haramu wa meno ya ndovu, iliopewa jina la Costa, iliingiza upelelezi uliofanywa Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Mkurugenzi wa idara ya wanyama pori katika Kenya, Julius Kipng'etich, alisema masoko ya kienyeji ya meno ya ndovu, viwanja vya ndege, vivuko vya mipakani na mahala kunakopitia biashara za magendo ndio yalikuwa malengo. Vitu vilivokamatwa ni ngozi za simba na bidhaa nyingine za magendo. Wachina watatu na Watanzania watatu ni miongoni mwa watu 65 waliokamatwa. Wengine ni raia wa Kenya.

Biashara ya meno ya ndovu ilipigwa marufuku tangu mwaka 1989, lakini biashara hiyo imeshamiri, hasa mahitaji yamezidi huko Mashariki ya mbali. Julius Kipng'etich anasema kwamba idadi ya ndovu katika Kenya, kama vile ile ya nchi nyingine za Kiafrika, inazidi kupungua kutokana na kuengezeka uwindaji haramu. Wawindaji haramu wanataka kuuza zaidi katika masoko ya kimataifa. Kukamatwa kukubwa hivi karibuni kwa meno ya ndovu yasiochongwa bado kunatoa dalili kwamba mengi ya meno hayo yanakusudiwa kusafirishwa hadi kwenye masoko ya Mashariki ya Mbali. Bwana Kipng'etich alisema operesheni za kusaka meno yaliopatikana kwa njia haramu bado inaendelea katika nchi hizo tano, nje ya Kenya, na kwamba matukeo zaidi yatatangzwa baade.

Peter Younger, mkuu wa mpango wa polisi wa kimataifa, Interpol, wa kusaidia operesheni dhidi ya uhalifu wa uwindaji haramu wa wanyama pori, mpango unaogharimiwa na serekali ya Ujerumani, amesema operesheni hiyo ilikuwa ya mafanikio makubwa, na utapelekea watu zaidi wakamatwe duniani. Alisema operesheni hiyo itaziwakilisha taasisi za kulinda sheria, katika Afrika na nje ya Afrika, ili kuzitambua njia zinazotumiwa na waendeshaji magendo, mawasiliano yao na mwishowe kupelekea kukamtwa watu wengine wanaohusika na uhalifu huo.

Keny imepoteza ndovu 200 mwaka huu waliouliwa na wawindaji haramu, ukilinganisha na 98 mwaka jana na 47 mwaka 2007.

Mkataba wa kimataifa juu ya biashara ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani, CITES, na unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ulizipa ruhusa serekali za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Botswana kusonga mbele kuuza kwa njia ya mnada wa siku moja pembe za ndovu zilizokusanywa katika mbuga zao za wanyama pori. Makundi yanayopigania haki za wanyama yalipinga biashara hiyo ya minada, yakisema kuuzwa kwa meno ya ndovu, hata ikiwa kwa njia halali, inachochea biashara ya magendo ya bidhaa hiyo, na hivyo uwinadaji haramu wa ndovu.

Idadi ya ndovu katika Kenya imezidi mara mbili, kufikia 30,000 tangu mkataba wa CITES kuipiga marufuku biashara ya meno ya ndovu. Hata hivyo, bado Kenya haijafikia idadi ya ndovu iliokuwa nayo kabla ya uwindaji haramu kuhatarisha kutoweka kabisa mnyama huyo nchini Kenya. Ilikadiriwa walikuweko ndovu 167,000 huko Kenya mwaka 1973.