Kimbunga Batsirai chasababisha vifo vya watu sita Madagascar
6 Februari 2022Shirika la kudhibiti majanga nchini humo limeeleza kwamba zaidi ya watu wengine 47,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na dhoruba iliyoleta mvua kubwa na upepo mkali usiku wa kuamkia Jumapili.
Mkurugenzi wa kitengo cha udhibiti wa hatari katika shirika hilo la kitaifa linaloshughulikia maafa nchini Madagascar, Paolo Emilio Raholinarivo, ameelezea juu ya maafa hayo kwenye ujumbe mfupi kwa shirika la Habari la AFP.
Baada ya kupata nguvu katika Bahari ya Hindi na vilevile kutokana na upepo mkali uliofikia kasi ya maili 145 kwa saa, kimbunga hicho kilipiga karibu na kisiwa cha Mananjary. Kwa mujibu wa idara ya hali ya hewa kisiwani humo, kwa sasa kasi ya upepo mkali imepungua hadi takriban maili 80 kwa saa.
Wakaazi wa kisiwa cha Mananjary na miji ya karibu ya Manakara na Nosy Varika wameelezea juu ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga hicho, wamesema mapaa ya nyumba yameezuliwa na miti pamoja na nguzo za umeme zimeangushwa hali inayofanya barabara kutopitika na kuyaacha maeneo mengi yakiwa yamefurika.
Sehemu nyingi nchini Madagascar zimejaa maji kutokana na dhoruba iliyotangulia inayoitwa Ana pia na mvua kubwa zilizonyesha mnamo mwezi Januari na hivyo kimbunga kipya Batsirai kinaongeza uharibifu na hali mbaya nchini Madascar.
Takriban watu 131,000 waliathiriwa na kimbunga Ana kote nchini Madagascar mwishoni mwa mwezi Januari. Takriban watu 60 walikufa, wengi wao katika mji mkuu wa Antananarivo. Kimbunga Ana pia kilizipiga Malawi, Msumbiji na Zimbabwe, na kusababisha vifo.
Idara ya hali ya hewa katika tarifa yake imesema kimbunga Batsirai kmeainishwa kama dhoruba hatari na kinatarajiwa kusababisha uharibifu mkubwa zaidi hasa mafuriko katika maeneo ya mashariki, kusini mashariki na nyanda za juu za kati, katika kisiwa cha Madagascar.
Mji mkuu wa Madascar, Antananarivo, ulipata mvua kubwa iliyonyesha kabla ya kimbunga Batsirai kupiga na kutokana na hofu wakaazi wameweka mifuko ya mchanga juu ya paa zao ili kuzilinda dhidi ya upepo. Na juu ya uharibifu uliotarajiwa, sehemu kubwa ya usafiri wa ardhini na wa baharini umesimamishwa nchini Madagascar, kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani.
Ofisi ya usimamizi wa hatari na maafa imesema takriban mikoa yote katika kisiwa hicho imo hatarini na imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kinawaweka hatarini takriban watu 600,000 kati ya jumla ya watu milioni 28 wa kisiwa hicho.
Idara ya huduma ya hali ya hewa ya Meteo ya Ufaransa ilikuwa imetabiri hapo awali kwamba kimbunga Batsirai kingesababisha maafa nchini Madagascar, baada ya kupita kwenye kisiwa cha Mauritius na kusababisha mvua kubwa kwenye kisiwa kinachodhibitiwa na Ufaransa cha La Reunion kwa muda wa siku mbili.
Soma zaidi:Baa la njaa latishia Madagascar
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limekadiria kwamba watu wapatao 595,000 wanaweza kuathiriwa moja kwa moja na kimbunga Batsirai, na wengine 150,000 zaidi wanaweza kupoteza makazi yao kutokana na maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Nayo mashirika ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu yamesema dhoruba hiyo inawaweka hatarini takriban watu milioni 4.4.
Vyanzo:AFP/AP