Korea Kaskazini yakanusha kubadilishana silaha na Urusi
17 Mei 2024Korea Kaskazini imekanusha na kutupilia mbali madai ya Marekani na Korea Kusini kwamba ilibadilishana silaha na Urusi. Hayo yameelezwa na Kim Yo Jong dada wa Kiongozi wa taifa hilo ambaye amesema tuhuma hizo ni za uzushi na upuuzi na kwamba silaha za Pyongyang ni kwa ajili ya ulinzi wake.
Hapo jana, Marekani iliwawekea vikwazo watu na makampuni kadhaa ya Urusi kwa kuwezesha usafirishaji wa silaha kati ya Urusi na Korea Kaskazini, ikiwa ni pamoja na makombora ya masafa marefu yanayotumiwa na Moscow nchini Ukraine.
Uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Urusi umeimarika kufuatia ziara ya Kim Jong Un nchini Urusi mnamo mwezi Septemba mwaka jana, ambapo alikutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin na kuahidi kuimarisha mahusiano yao ya kijeshi.