1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupanda thamani ya dola kwazusha wasiwasi duniani

18 Aprili 2024

Kuimarika kwa dola ya Marekani kunaibuwa wasiwasi mkubwa kwa mataifa ulimwenguni, na kuzusha kitisho sio tu katika nchi zinazoendelea kiuchumi bali pia katika nchi zilizoendelea kiviwanda.

https://p.dw.com/p/4ewTy
Sarafu ya dola
Thamani ya sarafu ya dola inazidi kupanda duniani.Picha: La Nacion/ZUMA/picture alliance

Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kupanda kwa asilimia 10% kwa sarafu ya dola kwenye soko la fedha kutapunguza pato la ndani la taifa katika nchi zinazoendelea kiuchumi kwa asilimia 1.9% baada ya mwaka mmoja, pamoja na athari mbaya za kiuchumi zinazodumu zaidi ya miaka miwili.

Karibu sarafu zote za  mataifa ya kundi la G20 yenye uchumi mkubwa na yale yanayoinukia kiuchumi zinashuka thamani dhidi ya dola.

Soma zaidi: Misri yapandisha bei ya mafuta kufuatia kushuka kwa thamani ya sarafu

Sarafu ya Lira ya Uturuki imekuwa ikiongoza kushuka thamani tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa 8.8%; Yen ya Japan imeshuka kwa asilimia 8% na Won ya Korea Kusini imeshuka kwa asilimia 5.5%.

Nchi zilizoendelea na zinazoibuka kiuchumi zimeshuhudia sarafu zikidhoofika kwa kasi, huku dola ya Australia, dola ya Kanada na euro ikishuka kwa asilimia 4.4%, 3.3% na 2.8%.

Dola inazidi kupata thamani
Wasiwasi huu sio tu kwa nchi zinazoendelea kiuchumi, Japan na nchi zingine zilizoendelea zina hofu kuhusu kuendelea kushuka kwa thamani ya sarafu zao.Picha: Patrick T. Fallon/AFP/Getty Images

Kimsingi, sababu kubwa iliyoko nyuma ya kuimarika kwa sarafu ya dola ya Marekani ni  kupungua kwa matumaini yaliyokuwepo ya kwamba huenda hivi karibuni Benki Kuu ya Marekani ingelipunguza viwango vya riba.

Sababu za kupanda kwa dola

Faharasa inayofuatilia bei za bidhaa muhimu nchini Marekani (CPI), ambayo ilichapishwa Jumatano (Aprili 17) ilionesha bei zimeongezeka kuliko ilivyotarajiwa katika masoko ya nchini humo, hali ambayo inamaanisha huenda viwango vya juu vya  mfumko wa bei nchini Marekani vikashuhudiwa tena.

Mipango ya Afrika Mashariki kuwa na sarafu moja

Na hilo litamaanisha benki kuu haitochukuwa hatua yoyote ya kupunguza riba.

Soma zaidi: Nusu ya makampuni ya Ujerumani yakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi

Pamoja na hayo, kuongezeka kwa msukosuko katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran dhidi ya Israel hivi karibuni, kumeiimarisha sarafu ya Marekani kuokana na kuwepo hali ya utulivu ndani ya Mareakani.

Dola ya Marekani
Thamani ya sarafu ya dola ya Marekani inazidi kuimarika.Picha: picture alliance/imageBROKER

Hatimaye, wakati uchumi duniani kote unakabiliwa na ukuaji wa wastani, viashiria vya kiuchumi vya Marekani, kuanzia takwimu za ajira hadi mauzo ya rejareja, vinaendelea kuzidi matarajio.

Athari kwa mataifa yanayoendelea

Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na athari mbaya kutokana na kupanda kwa dola, kwa sababu kuongezeka kwa thamani ya sarafu hiyo husababisha ongezeko la riba kwa deni lao linalolipwa kwa dola, hivyo kuwaongezea mzigo wa riba.

Mwanzoni mwa mwaka 2024, wengi waliamini kwamba viwango vya riba vya Marekani vitapunguzwa kufikia mwishoni mwa mwaka. Lakini sasa dola inaonekana kuimarika kwa kasi kuliko ilivyotarajiwa.

Soma zaidi: Pato la taifa Ujerumani kunywea hadi asilimia 0.5 mwaka 2023

Masoko yanayoibukia tayari yako katika hali ya mgogoro.

Mnamo Aprili Mosi, Benki Kuu ya Brazil iliingilia kati soko la fedha za kigeni nchini humo kwa mara ya kwanza tangu Rais Luiz Inacio Lula da Silva aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2023. 

Alama ya sarafu ya Yuan ya China.
Alama ya sarafu ya Yuan ya China.Picha: Chris Clor/Blend Images/picture alliance

Benki ya Indonesia (BI) imekuwa ikiingilia kati ili kupata sarafu yake ya rupia, ambayo iko katika kiwango cha chini kuwahi kufika katika miaka minne.

Gavana wa benki hiyo, Perry Warjiyo, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuhudhuria mkutano na Rais Joko Widodo siku ya Jumanne, kwamba benki kuu "daima iko sokoni na itahakikisha kuwa sarafu hiyo ni thabiti."

Benki Kuu ya Uturuki pia ilipandisha kiwango cha sarafu yake kwa 5% hadi 50% mwezi Machi ili kukabiliana na kushuka kwa thamani ya lira na kuongeza kasi ya mfumuko wa bei.

Hofu kwa mataifa yaliyoendelea

Wasiwasi huu sio tu kwa nchi zinazoendelea kiuchumi tu. Japan na nchi zingine zilizoendelea zina hofu kuhusu kuendelea kushuka kwa thamani ya sarafu zao.

Euro
Sarafu ya euro ya mataifa ya Ulaya nayo inazidi kupoteza thamani mbele ya dola ya Marekani.Picha: Bekim Shehu/DW

Kama anavyoeleza Kota Hirayama, afisa katika kampuni inayoshughulikia masuala ya fedha, SMBC Nikko Securities, "hatari ya kurejea kwa mfumuko wa bei inaongezeka katika nchi zinazoibuka kiuchumi" kwa sababu ya viwango vya ubadilishaji fedha na kupanda kwa bei ya mafuta.

Soma zaidi: Marekani yaishauri Nigeria kuwa na sarafu imara

Kupitia barua kwa wawekezaji, mtaalamu alieleza kuwa kuna uwezekano wa kutoongezeka viwango vya riba, na badala yake wafanye mabadiliko ya sera ya fedha ili kukabiliana kwa muda na kushuka kwa thamani ya sarafu zao.

China, kwa mfano, inatumia uwekaji fedha wake wa kila siku kusaidia Yuan, na baadhi ya benki zinazomilikiwa na serikali zinauza akiba ya dola.

Benki ya Indonesia, taifa linaloinukia kiuchumi, nayo inafanya vivyo hivyo.

Imekusanywa na Wakio Mbogho