Lebabon: Israel haitaki kusitisha vita
1 Novemba 2024Shirika la habari la taifa la Lebanon limeripoti kuwa mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo yaliyolengwa, huku majengo kadhaa yakigeuzwa vifusi, pamoja na kuzuka kwa moto na kuongeza kuwa mashambulizi pia yalilenga mji wa Aley, ambao upo kusini mashariki mwa mji mkuu, na mwingine Bint Jbeil kusini mwa nchi.
Jeshi la Israel limesema linaendelea na operesheni dhidi ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran nchini Lebanon na mshirika wake wa Kipalestina Hamas katika Ukanda wa Gaza. Mashambulizi hayo yametokea siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukutana na maafisa wa Marekani kujadili uwezekano wa makubaliano ya kumaliza vita nchini Lebanon, kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani wa Jumanne ijayo.
Lebanon imelaani mashambulizi ya Israel katika ardhi yake
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amelaani kupanuka kwa mashambulizi ya Israel, akisema kunaashiria kukaidi kushiriki katika juhudi za usuluhishi.
Taarifa zinasema mashambulizi hayo yalilenga maeneo ya Ghobeiry, Al-Kafaat, Barabara Kuu ya Sayyed Hadi, na eneo karibu na Al-Mujtaba Complex na barabara ya zamani ya uwanja wa ndege. Israel imezidisha mashambulizi yake ya mabomu kusini mwa Beirut huku pia ikifanya mashambulizi mabaya kwingineko nchini Lebanon.
Kwa upande mwingine Margaret Harris ni Msemaji wa Shirika la Afya Duniani, WHO anasikitikia kutatizwa kwa huduma ya afya "Kwa kweli, tuna wasiwasi sana, tuna wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa afya na vituo vya Lebanon, na tunasisitiza tena na tena kwamba huduma isilengwe, watoa huduma ya afya wasishambuliwe. Na tuna wasiwasi kuona mkondo sawa na ule wa mashambulizi ya Israel huko Gaza." Alisema afisa huyo.
Wachambuzi waonesha hofu ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita
Wachambuzi wanasema mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yanasababisha ugumu wa kufikia makubaliano. Siku ya Alhamisi, Netanyahu aliwaambia wajumbe wa Marekani Amos Hochstein na Brett McGurk kwamba makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano na Hezbollah lazima yahakikishe usalama wa muda mrefu wa Israel.
Ndani katika eneo la Gaza, maafisa wanasema idadi ya waliokufa kutokana na mashambulizi ya mapema leo, katikati ya eneo hilo imefikia watu 25. Idadi hiyo inajumuisha watoto watano na wanawake 7. Israel haijasema lolote kuhusu shambulizi husika lakini imesema imewaua wapiganaji katika eneo hilo la kati la Gaza.
Soma zaidi:Matumaini ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah
Hayo yanatokea katika wakati huu ambao pia wizara ya afya huko Gaza inayoratibiwa na Hamas ikisema takriban watu 43,259 wameuawa katika vita hivyo vilivyodumu kwa mwaka sasa. Idadi hiyo inajumuisha vifo 55 vilivyotokea katika kipindi cha saa 24 zilizopita.