1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LHRC: Wafungwa na walio nje Tanzania washiriki uchaguzi.

Admin.WagnerD21 Novemba 2023

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) -21.11.2023- kimeibua kilichoyaita kuwa ni mapungufu katika miswada ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

https://p.dw.com/p/4ZGKc
Tansania Dr. Tulia Ackson
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Katika mapendekezo yake kituo hicho kinataka sheria za uchaguzi zijumuishe wafungwa kupiga kura katika uchaguzi wa rais na wabunge huku wakisisitiza kupatikana kwa katiba mpya.

Muswada wa sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi, muswada wa sheria ya uchaguzi wa rais na wabunge na muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa iliwasilishwa Novemba 10 bungeni na kufungua pazia pana la mabadiliko katika chaguzi za kisiasa hapa nchini.

Takwa la uchaguzi huru na haki Tanzania

Afrika Tansania Dar es Salaam Wahlen
Mpiga kura akishiriki haki yake ya msingi katika uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2020Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Hata hivyo tangu kufunguliwa kwa pazia hilo, wadau mbalimbali wa kisiasa na utawala bora, wametoa maoni yao, baadhi wakipongeza na wengine wakitaka maboresho ili sheria hizo zikidhi chaguzi huru na haki.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) wamefanya uchambuzi wa miswada hiyo kabla ya kuwa sheria kamili na kubaini mapungufu kadhaa, ikiwamo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, watumishi wa umma kuwa sehemu ya tume ya uchaguzi na tume kuendelea kutegemea bajeti ya serikali.

Pendekezo la Watanzania waishio nje ya nchi kupiga kura

Kadhalika, kituo hicho kilipendekeza muswada wa sheria ya uchaguzi kutoa haki kwa jumuiya ya watanzania waishio nje ya nchi, kupata haki ya kupiga kura. Pamoja na hayo wakasisitiza wakisema katiba mpya ndiyo suluhisho la kudumu la demokrasia Tanzania.

Pamoja na LHRC wachambuzi wengine wa siasa, wamechambua miswada hii na kupongeza lakini wakiitaka serikali kutilia mkazo suala la katiba mpya na wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu basi suala la tume huru ya uchaguzi lisifanyiwe mzaha.

Soma zaidi:Tanzania yakosolewa oparesheni kukomeshai ukahaba

Tume ya taifa ya uchaguzi na sheria za uchaguzi ni miongoni mwa vipengele vinavyolalamikiwa zaidi na wanasiasa nchini hapa hali iliyopelekea baadhi kufungua kesi mahakamani kuipinga sheria ya sasa ya uchaguzi na kutaka mabadiliko ya katiba mpya, hivyo basi kuwasilishwa kwa miswada hii kumewaibua wadau hawa wa siasa na haki za binadamu katika  kipindi ambacho taifa hili la Afrika Mashariki linaelekea katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, 2025 na wa serikali za mitaa, 2024.

DW. Dar es Salaam