Libya: Umoja wa Mataifa walaani uvamizi wa majengo ya bunge
3 Julai 2022Waandamanaji walilivamia bunge katika mji wa mashariki wa Tobruk siku ya Ijumaa usiku na walivamia ofisi za baraza la wawakilishi na kisha kuchoma sehemu ya jengo hilo.
Katika mji mkuu wa eneo la mashariki, Benghazi eneo ambalo ni kitovu cha uasi wa mwaka 2011 na kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, maelfu ya waandamanaji waliingia mabarabarani kudai kurudishwa kwa huduma za umeme na kuzorota kwa hali ya maisha kwa jumla. Wengine walipeperusha bendera za kijani za utawala wa zamani wa rais aliyeondolewa madarakani na kishan kuuawa Muammar Gadhafi. Maandamano pia yalifanyika katika mji mwingine wa Misrata.
Utulivu ulionekana kurejea katika jiji la Tobruk jana Jumamosi, ingawa kulikuwa na miito kwenye mitandao ya kijamii wa kuhimiza maandamano zaidi.
Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katibu mkuu ametoa wito kwa pande zote kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kudhoofisha uthabiti nchini Libya na amewataka wahusika kushirikiana pamoja ili kuondokana na mkwamo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams amelaani uvamizi huo katika majengo ya bunge uliofanywa na waandamanaji wenye hasira na kusema kuwa vitendo vya uharibifu havikubaliki kabisa.
Machafuko Libya
Libya imetumbukia katika machafuko tangu vuguvugu lililoungwa mkono na Jumuiya ya kujihami ya NATO, kumwondoa madarakani rais wa muda mrefu Muammar Gadaffi mwaka 2011. Kwa miaka kadhaa nchi hiyo imegawanyika katika tawala mbili hasimu upande wa mashariki na magharibi, zote zikiungwa mkono na makundi tofauti ya wapiganaji na serikali za kigeni.
Mazungumzo ya upatanishi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva wiki hii yaliyolenga kuvunja mkwamo kati ya pande hasimu za Libya hayakufaulu kutatua tofauti kuu kati ya pande hizo.
Waziri mkuu wa mpito Abdulhamid Dbeibah anaongoza utawala wenye makao yake makuu mjini Tripoli huku waziri wa zamani wa mambo ya ndani Fathi Bashagha akipata uungwaji mkono kutoka kwa baraza la wawakilishi lenye makao yake mjini Tobruk na jenerali wa eneo la mashariki Khalifa Haftar.
Vikosi vya Haftar vimesema vinaunga mkono madai ya raia lakini vimewataka waandamanaji kuheshimu mali ya umma.
Mtaalamu wa maswala ya Libya Jalel Harchaoui ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja, juhudi nyingi za kidiplomasia na za upatanishi nchini Libya zimetawaliwa na wazo la kufanyika uchaguzi, ambao hautafanyika kwa angalau miaka miwili, kutokana na kushindwa kwa mazungumzo ya mjini Geneva.
Mjumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Libya, Jose Sabadell, amesema matukio ya Ijumaa yanathibitisha kwamba watu wa Libya wanataka mabadiliko kupitia uchaguzi.
Balozi wa Marekani nchini Libya Richard Norland amesema hakuna upande mmoja wa kisiasa utakaofurahia udhibiti halali katika nchi nzima ya Libya na jitihada zozote za kuweka utawala wa upande mmoja zitasababisha ghasia nchini humo.
Balozi Norland amewataka viongozi wa kisiasa wa Libya na nchi za kigeni zinazowaunga mkono kuutumia wakati huu kurejesha imani ya raia wa Libya kwa ajili ya mustakabali wa nchi hiyo.
Chanzo: AFP