Libya: Pande mbili hasimu zatia saini mkataba wa amani
24 Oktoba 2020Umoja wa Mataifa umeyaita makubaliano hayo kuwa ya kihistoria baada ya mapigano ya miaka kadhaa yaliyoigawanya Libya katika pande mbili. Pamoja na hatua nyingine, makubaliano hayo yanaagiza kuondolewa kwa mamluki wa kutoka nje na kuwezesha kufanyika mazungumzo mwezi ujao ili kutafuta suluhisho la kudumu.
Libya ilitumbukia katika vurumai baada ya nchi za NATO kuivamia nchi hiyo mnamo mwaka 2011 na kumwondoa kiongozi wake kanali Muammar Gaddaffi aliyetawala kwa muda mrefu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema makubaliano yaliyofikiwa ni muhimu sana, hata hivyo ameeleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika.
Mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mgogoro wa Libya, Stephanie Williams amesema makundi yenye silaha na vikosi vya kijeshi vimekubali kurejea kwenye kambi zao na kwamba makubaliano yaliyofikiwa yataanza kutekelezwa mara moja.
Shirika la Mafuta la Kitaifa la Libya (NOC) limetangaza kuanza tena kwa usafirishaji wa mafuta kutoka kwenye vituo viwili muhimu mashariki mwa nchi hiyo baada ya pande zinazopingana kuzatangaza kuwa zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Shirika la Mafuta la Kitaifa lemesema limepokea uthibitisho kwamba vikosi vya kigeni vimeondoka kutoka kwenye eneo la bandari hatua itakayoliwzesha shirika hilo kufanya shughuli zake za kuchimba mafuta na kuanza kuuza nje. Vituo hiyvo viwili muhimu vya kuzalisha mafuta ghafi ni Ras Lanuf na Al-Sidra, ambavyo vilikuwa vinadhibitiwa na Jenerali Khalifa Haftar.