1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Livni kukabiliwa na kizingiti mchakato wa amani Mashariki ya Kati

Josephat Nyiro Charo21 Februari 2013

Makubaliano ya Muungano wa waziri wa sheria mteule wa Israel, Tzipi Livni, na waziri mkuu, Benjamin Netanyahu, unatoa sura juu ya changamoto nyingi zitakazomkabili katika jukumu lake jipya

https://p.dw.com/p/17ix9
Israel's Prime Minister Benjamin Netanyahu (L) and former Foreign Minister Tzipi Livni, head of the centrist Hatenuah party, deliver a joint statement at the Knesset, the Israeli parliament, in Jerusalem February 19, 2013. Netanyahu took his first step in forming a new government on Tuesday saying he had signed a coalition deal with Livni, who will handle efforts to renew stalled Middle East diplomacy. REUTERS/Ronen Zvulun (JERUSALEM - Tags: POLITICS)
Israel Zipri Livni Koalition Benjamin Netanjahu Pressekonferenz KnessetPicha: Reuters

Katika hatua yake ya kwanza ya kuunda serikali baada ya uchaguzi wa Januari 22 mwaka huu, Netanyahu alitangaza Jumanne wiki hii kwamba Tzipi Livni atakuwa waziri wa sheria na kushughulikia juhudi za kuyaanzisha tena mazungumzo ya amani na Wapalestina, yaliyokwama tangu mwaka 2010.

Hisia mbalimbali ziliibuka kutoka kwa Wapalestina, huku baadhi ya maafisa wakisema wangelipendelea kuona muundo kamili wa serikali mpya ya Netanyahu. Huku uteuzi wa Livni kama mpatanishi ukionekana kuashiria jitihada mpya za kutafuta amani, maswali yamezuka kama kiongozi huyo atakuwa tu kama mtu wa kujaribu kuficha aibu za Netanyahu, ambaye sera yake ya ujenzi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi ndio umekuwa suala nyeti katika mkwamo huo.

Ziara ya Obama

Matarajio ya kuanza kwa mchakato mpya wa amani yameongezeka kutokana na ziara ya rais wa Marekani, Barack Obama, atakayeitembelea Israel, eneo la Ukingo wa Magharibi na Jordan mwezi ujao.

U.S. President Barack Obama speaks during a news conference at the White House in Washington, January 14, 2013. REUTERS/Jonathan Ernst (UNITED STATES - Tags: POLITICS)
Rais Barack ObamaPicha: Reuters

Yosi Verter, mchambuzi wa siasa wa gazeti la mrengo wa shoto la Israel, Haaretz, aliandika katika toleo la Jumatano kwamba Netanyahu atamtumia Livni kutangaza sera za Israel katika nchi za kigeni na Netanyahu atamtuma kwa Wamarekani na Wazungu ambao wanampenda, ili aeleze ugumu wa maisha ya muungano wa kisiasa na vipi suala la Wapalestina halipewi kipaumbele.

Abdallah Abdallah, afisa wa cheo cha juu wa chama cha Fatah cha rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abaas, amesema, " Natumai uteuzi wa Livni si hatua ya kimkakati kwa upande wa Netanyahu katika kujiandaa kwa ziara ya rais Obama."

Waziri wa ulinzi wa Israel anayeondoka, Ehud Barak, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiitsha mazungumzo na Wapalestina, alikuwa kwa kiwango kikubwa akitazamwa kama mtu mwenye jukumu la kufunika aibu kwa niaba ya Netanyahu. Uhusiano wa waziri mkuu na rais Obama unaokabiliwa na mtihani, umeangazia tofauti zilizopo baina yao kuhusu sera ya ujenzi wa makazi na jinsi ya kuuzuia mpango wa nyuklia wa Iran.

Wapalestina hawataki mazungumzo

Wapalestina wamekataa katakata kuendelea na mazungumzo na Israel kama haitosita kujenga makazi ya walowezi, ambayo wanasema yanachukua sehemu kubwa ya ardhi wanayoihitaji kwa ajili ya taifa lao huru. Netanyahu ameshawahi kusema kwamba yuko tayari kwa mazungumzo bila masharti yoyote.

"Livni ana uzoefu katika mashauriano ya amani, lakini la muhimu zaidi ni uamuzi wa kisiasa atakaoutekeleza. Na huo unategemda sera ya serikali ya bwana Netanyahu," amesema Abdalla Abdalla wa chama cha Fatah.

Israel na Marekani pia zimekuwa na matumaini madogo juu ya uwezekano wa kupatikana ufanisi katika juhudi za kuunda taifa huru la Palestina, ambalo Netanyahu anasema lazima lisiwe na silaha wala kuwa kitisho kwa usalama wa taifa hilo la Kiyahudi.

Alipoulizwa kwenye mahojiano na redio ya jeshi la Israel Jumatano wiki hii, kama Netanyahu amemuahidi chochote kuzuia ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, Livni alisema suala la kuyafufua tena mazungumzo ya amani ni nyeti. Livni pia alisema baada ya serikali mpya kuundwa, atatilia maanani kinachohitajika ili kuyaanzisha tena mazungumzo hayo, masharti yatakayokuwepo na misimamo ya Marekani, Ulaya na Wapalestina wenyewe.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf