Liz Truss ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza
6 Septemba 2022Liz Truss mwenye umri wa miaka 47, leo ameshika rasmi hatamu ya uongozi na kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza baada ya kukutana na Malkia Elizabeth wa Pili mwenye umri wa miaka 96 katika kasri lake lililopo Balmoral, Scotland.
Kabla ya tukio hilo Boris Johnson, aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye alilazimishwa kujiuzulu kufuatia utawala wake wa miaka mitatu uliojaa misukosuko, alitoa hotuba yake ya mwisho na pia akampelekea malkia barua yake ya kujiuzulu rasmi.
Truss ambaye kabla ya cheo chake kipya alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, amekuwa Waziri mkuu wa nne wa Uingereza katika kipindi cha miaka sita iliyopita, lakini Waziri mkuu wa 15 katika kipindi cha miaka 70 tangu Elizabeth wa Pili kuwa Malkia.
Soma pia:Maoni: Urithi wenye sumu wa Brexit anaoacha Theresa May
Kulingana na taarifa kutoka makao makuu ya Malkia iliyoko Buckingham, Malkia alimteua na kumruhusu Truss kuunda serikali mpya. Hii ni mara ya kwanza ukabidhiaji madaraka umefanyika katika makao ya Malkia iliyoko Balmoral tangu mwaka 1885, wakati malkia Victoria ndiye alikuwa usukani.
Truss anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza kwa umma kama waziri mkuu wakati wowote jioni hii.
Miongoni mwa majukumu yake ya kwanza ni kuteua mawaziri kumsaidia kukabili changamoto mbaya za kiuchumi ambazo hazijawahi kuikumba nchi hiyo kwa miongo mingi, ikiwemo mfumuko wa bei za bidhaa kupanda maradufu na kodi za nishati kupanda.
Uteuzi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mkutano wake wa kwanza wa baraza la mawaziri na kufika mbele ya bunge kujibu maswali kesho Jumatano.
Boris Johnson ang'aa kumrithi May
Truss anayejichukulia kama Mliberali wa soko huru, ameahidi kupunguza kodi kama chachu ya maendeleo.
Vyombo vya Habari vya Uingereza vimeripoti leo kwamba atasimamisha tozo za nishati kwa kaya na biashara zinazolemewa na gharama ya maisha, hatua inayoweza kuigharimu serikali dola bilioni 116.
Hata hivyo, uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na shirika la YouGov umeonesha kwamba 14% pekee ya Waingereza ndio wana matumaini kwamba Truss atafanya vyema kuliko mtangulizi wake Boris Johnson.
(Vyanzo: RTRE, AFPE)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Grace Patricia Kabogo