1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya Corona yaongezeka Ulaya na Amerika Kusini

11 Oktoba 2020

Ujerumani na Poland zimeweka upya karantini ili kudhibiti kuenea maambukizi ya virusi vya corona wakati idadi ya watu wanaoambukizwa ikiongezeka barani Ulaya,

https://p.dw.com/p/3jkYl
Neue Corona-Regeln Frankfurt am Main
Picha: Frank Rumpenhorst/dpa/picture alliance

Karantini imewekwa upya katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin ambao ni maarufu kwa pilikapilika za usiku kama jitihada ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona. Migahawa na baa vitafungwa saa tano usiku, katika marufuku ambayo itadumu hadi Oktoba 31. Hatua kama hiyo imechukuliwa katika mji Frankfurt, lakini utekelezaji wake utaanza saa nne usiku.

Kukiwa na maambukizi ya zaidi ya watu 400 kwa siku mjini Berlin, ufungaji wa maeneo hayo ya biashara unahusu maduka yote isipokuwa maduka ya madawa na vituo vya kuuzia mafuta ingawa havitaruhusiwa kuuza pombe.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel tayari alikuwa ameonya sku ya Ijumaa kuwa maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi yataangaliwa kwa muda wa siku 10 kuona kama maambukizi yatapungua la sivyo hatua madhubuti zitachkuliwa ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi na aliitaka miji mikubwa iongeze kasi ya kulidhibiti janga la corona. Katika nchi jirani ya Poland, viongozi wanawasisitizia watu wavae barakoa katika maeneo yote ya umma baada ya maambukizi mapya ya virusi vya corona kwa siku moja kupindukia watu 4,280 waliomabukizwa.

Katika Jamuhuri ya Czech matarajio ya kuwekwa vizuizi vipya yanapewa kipaumbele kutokana na kuongezeka kwa maradhi ya COVID -19. Serikali mbalimbali barani Ulaya zinajitahidi kudhibiti kuongezeka kwa maambukizi wakati huu wa wimbi la pili la janga la corona linalotokea huku msimu wa mafua makali (Influenza) ukiwa unasubiriwa.

Madaktari kwenye chumba cha watu mahututi wanaougua COVID -19 nchini Ufaransa
Madaktari kwenye chumba cha watu mahututi wanaougua COVID -19 nchini UfaransaPicha: Christophe Simon/AP Images/picture-alliance

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa mara ya kwanza idadi ya kila siku barani Ulaya ya maambukizi ya virusi vya corona imefikia watu 100,000. Uhispania hasa ndiyo iliyoathirika zaidi kutokana na maambukizi hayo. Serikali ya Uhispania imetangaza hali ya dharura katika mji wake mkuu wa Madrid.

Miji kadhaa ya Ufaransa tayari imeshashuhudia idadi ya kupindukia ya maambukizi hayo. Nchini Uholanzi, zaidi ya maambukizi mapya ya watu 6,000 yaliripotiwa, huku idadi ya wagonjwa ikiwa inaongozeka mahospitalini.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Tom Brenner/Reuters

Wakati huo huo daktari wa ikulu ya Marekani, kamanda Sean Conley amesema, Rais Donald Trump hayumo tena katika kitisho cha kuweza kuambukiza virusi vya corona. Taarifa hiyo ya uchunguzi wa kitabibu imetolewa katika kipindi ambacho rais Trump anajiandaa kuanzisha upya kampeni na shughuli zingine.

Taarifa ya daktari huyo inasema Trump ametimiza vigezo vya usalama kulingana na Kituo cha Udhibiti na Kinga (CDC) kwa hiyo hayumo katika hatari ya kuweza kueneza maambukizi. Hata hivyo taarifa hiyo haijasema kama kiongozi huyo kapimwa na kuonekana hana virusi hivyo.

Taarifa hiyo imetolewa  baada ya rais Trump kuonekana kwa mara ya kwanza mbele ya umma tangu aliporudi ikulu baada ya kutibiwa ugonjwa wa COVID -19. Mamia ya watu walikusanyika siku ya Jumamosi alasiri kwenye eneo la wazi la Kusini mwa ikulu wakati ambapo rais Trump akiwa kwenye roshani aliwahutubia na kusisitiza kuhusu anavyowaunga mkono maafisa wa usalama nchini Marekani.

Vyanzo:/AFP/APE

Mhariri: Sudi Mnette