1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron aomba msamaha kufuatia mauaji ya kimbari Rwanda

27 Mei 2021

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ametambua jukumu la nchi yake katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na anatumai wahanga wa mauaji hayo wataisamehe Ufaransa.

https://p.dw.com/p/3u3VQ
Ruanda | Rede Emmanuel Macron in Kigali
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Macron ameyasema hayo mjini Kigali katika ziara inayotarajiwa kurekebisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, baada ya miaka mingi ya shutuma za Rwanda kwamba Ufaransa ilihusika katika mauaji hayo

Akizungumza katika eneo la makumbusho la Gisozi mjini Kigali, kulikozikwa zaidi ya wahanga 250,000 wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Macron amesema wale waliopitia ''usiku'' wa mauaji hayo ndio wanaoweza labda kusamehe na kutoa zawadi ya msamaha kwa Ufaransa. " Nasimama hapa kwa unyenyekevu na heshima kubwa na nimekuja kutambua ukubwa wa dhima yetu," aliongeza kusema rais Macron.

Ziara ya rais huyo wa Ufaransa, inafanyika baada ya ripoti iliyochapishwa mwezi Machi mwaka huu kutoka kwa  jopo la uchunguzi la Ufaransa lililohitimisha kuwa mtazamo wa kikoloni uliwafumba macho  maafisa wa Ufaransa, kwa hiyo serikali ya nchi hiyo inabeba lawama kubwa kwa kutotambua mauaji hayo. Lakini ripoti hiyo haikuihusisha moja kwa moja  Ufaransa na mauaji ya zaidi ya watu 800,000 wa kabila la watutsi pamoja na watu wa kabila la wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani.

soma zaidi: Macron alenga kuanzisha upya mahusiano na Rwanda

Macron ameongeza kuwa wauwaji waliovamia misitu, milima na makanisa hawakuwa na sura za ufaransa na kwamba ufaransa haikula njama ya kushiriki katika mauaji hayo. Jean Paul Kimonyo msaidizi wa zamani wa rais wa Rwanda Paul Kagame, amesema hotuba ya Macron ilikuwa na uzito maana ameomba msamaha kwa unyenyekevu.

Kagame asema wanyarwanda huenda wasisahau kilichotokea lakini wanaweza kusamehe

Kigali | Macron Besuch in Ruanda
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: AFP

Rais Paul Kagame ambaye awali aliwahi kusema kuwa Ufaransa ilihusika katika mauaji ya Kimbari, wiki iliyopita alisema ripoti iliyotolewa mwezi Machi ilikuwa na maana kubwa sana kwa watu wa Rwanda. Kagame amesema ukweli siku zote unapoza kidonda, na kwamba hakuna njia fupi kwa hiyo Ufaransa ni lazima ifuate mkondo huo huo. 

"Wanyarwanda huenda wasisahau kilichotokea lakini wanaweza kuisamehe Ufaransa kwa jukumu lake," alisema rais Kagame anaetokea kabila la watutsi na mtu aliye na nguvu kubwa katika siasa za Rwanda tangu jeshi lake lilipositisha mauaji ya kimbari yaliokuwa yanaendeshwa na wanamgamboi waliokuwa tiifu kwa serikali iliyoongozwa na wahutu.

soma zaidi:  Macron atambua dhima ya Ufaransa katika mauaji ya Rwanda

Macron, ambaye alijaribu kuitenga Ufaransa na majukumu yake ya kikoloni alikubali mwezi Aprili kufungua mafaili ya uongozi wa rais wa zamani Francois Mitterrand, aliyekuwa rais wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Muda mfupi baadaye Rwanda nayo ikatoa ripoti yake iliyogundua kuwa Ufaransa ilifahamu kuwa mauaji ya kimbari yalikuwa yanapangwa kutekelezwa na imechukua jukumu kwa kukubali mauaji hayo kufanyika bila ya kuchukua hatua yoyote ya kuyasimamisha na kuendelea kumuunga mkono rais wa wakati huo Juvenal Habyarimana.

Kuangushwa kwa ndege ya rais Habyarimana ndiko kuliko washa moto Rwanda

Ruanda Juvenal Habyarimana Flugzeug 1994 Archiv
Mabaki ya ndege iliyodunguliwa mwaka 1994 ya rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana Picha: AP

Kudunguliwa kwa ndege iliyokuwa imembeba rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarimana kulifungua uwanja wa siku 100 wa mauaji mabaya kuwahi kushuhudiwa Rwanda.

"Maafisa wa Ufaransa, waliwapa silaha, ushauri, mafunzo na kuilinda serikali ya Rwanda ilisema ripoti hiyo ya Rwanda na kuongeza kuwa Ufaransa ilificha jukumu lake katika mauaji hayo kwa miaka mingi.

soma zaidi: Rwanda yailaumu Ufaransa kushindwa kuzuia mauaji ya Kimbari

Siku ya Ijumaa Kasri la Elysee lilisema kuwa Macron atamtangaza balozi wa Ufaransa nchini Rwanda akijaza nafasi iliyowachwa wazi tangu mwaka 2015.

Macron ni rais wa hivi karibuni kufanya ziara nchini Rwanda, ziara ya mwisho ilifanyika mwaka 2010.

Baada ya Rwanda rais huyo wa Ufaransa anatarajiwa kwenda Afrika Kusini atakakokutana na rais Cyril Ramaphosa kujadili changamoto za COVID 19 kwa taifa hilo na migogoro mingine ya kikanda ikiwemo hali nchini Msumbiji.

 Vyanzo: ap/reuters